Kocha aliefukuzwa Boris Bunjak |
Aliyekuwa Kocha wa Azam Stewart Hall |
KOCHA Mserbia wa Azam FC, Boris Bunjak amefukuzwa rasmi leo na sasa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall anarudishwa kazini.
Habari kutoka ndani ya Azam FC zimesema kwamba, sababu za kufukuzwa kwa Mserbia huyo ni kushuka kwa kiwango cha timu, hali iliyosababisha sasa ianguke hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Tayari Bunjak amekwishapewa haki zake zote na ataondoka Alhamisi, siku ambayo Stewart atawasili kuanza tena kazi Azam FC.
Bunjak anaondoka Azam baada ya kuiongoza timu katika mechi 16, akifungwa nne tu, zote dhidi ya Simba ikiwemo ya juzi ya Ligi Kuu, waliyofungwa 3-1 na kutoa sare tatu
Bunjak mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), alitua Azam, Agosti 7, mwaka huu akitokea FC Damac ya Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na kabla ya hapo alifundisha klabu kibao za kwao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK Javor Ivanjica, Crvena Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK Mladi Radnik, FK Crvena Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
Awali, Bunjak aliyezaliwa Novemba 17, mwaka 1954 ( miaka 57), alicheza soka katika klabu za FK Sloga (Kraljevo), FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki (Kragujevac), FK Olimpia (Ljubljana), FK Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo), FK Borac (Cacak) na FK Sloga (Kraljevo).
Stewart alifukuzwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano kufukuzwa Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini Stewart angalau aliacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame miezi miwili iliyopita, mambo ambayo bila shaka yamemfanya afikiriwe tena.