Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania (ILO) Bw. Alexio Musindo akikagua kinywaji aina ya ‘paw paw wine’ na mkononi akiwa ameshika matunda aina ya ‘rozela’ yanayotumika kwa kutengenezea ‘juice’ wakati alilipotembelea kikundi cha Chimbuko kinachoundwa na watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Mjini Kyela mnamo tarehe 2, Aprili 2013 ili kujua maendeleo yao. Kikundi cha Chimbuko ni moja kati ya vikundi vya kijamii vinanvyonufaika na mradi wa UKIMWI kwa njia ya uwezeshaji Kiuchumi unaoratibiwa na ILO katika maeneo ipitayo njia kuu ya Tanzania – Zambia. (yaani Chalinze, Ilula, Mafinga, Makambako, Kyela na Tunduma).
Mwenyekiti wa kikundi Cha Chimbuko Bi Sara Mwakinyuke akimwelezea Ndugu Alexio Musindo, Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania kuhusu matumizi ya bidhaa aina Rozela. Alifafanua pia miongoni mwa bidhaa wanazotengeneza ni pamoja na mmea wa asili aina ya mlonge ambapo alisema mlonge hutumika kama dawa inayotibu malaria. Kushoto kwake ni Afisa Mratibu Mkuu wa ILO nchini Tanzania Ndugu Anthony Rutabanzibwa aliyeongozana na Mukurugenzi wa ILO katika ziara hiyo.
Miongoni mwa vitu vilivyowashangaza maafisa wa ILO walipotembelea kikundi cha Chimbuko ni mmea wa Rozela na matunda yake kwani miongoni mwao hawajawahi kuona mmea huo bali matunda yake yakiwa tayari yameshahifadhiwa katika vifungashio. Sambamba nalo ni kitafunwa aina ya keki ya muhogo ambayo Mkurugenzi wa ILO kanda ya Afrika Mashariki alishangazwa baada ya kula keki hiyo namna ambavyo hata unga wa muhogo pia unaweza kutengenezwa keki na ikawa tamu kwelikweli!
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani Kanda ya Afrika ya Mashariki nchini Tanzania Ndugu Alexio Musindo akiangalia bidhaa aina ya unga uitwao ‘SHIBE’ wenye mchanganyiko wa ulezi, soya lishe, mchele, karanga na mahindi unaosindikwa na kikundi cha chimbuko kama lishe bora inayoweza kutumiwa na watu wa rika zote wakiwemo wanaoishi na VVU na UKIMWI, wazee na watoto
Mwenyekiti wa vikundi cha Chimbuko Bi. Sara Mwakinyuke akimwelezea Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania juu ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika kujipatia kipato kupitia bidhaa wanazozalisha ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifungashio kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha, kutoshiriki katika maonyesho ya Kitaifa ya biashara na ujasiriamali na kukosa elimu ya kutosha kuhusu uzalishaji wa bidhaa zao. Ndugu Alexio Musindo aliwaahidi kuwawezesha kupata vifungashio na Uongozi wa Halmashauri ya Kyela kupitia idara ya UKIMWI kuwaahidi kuwawezesha ili washiriki katika maonyesho ya saba saba mwaka 2013 yatakayofanyika mjini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kikundi cha wanawake wajasiriamali cha Faith kilichopo Mjini mbeya Bi Helene Sanga akifafanua jambo baada ya kutembelewa na Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania mnamo tahere 2 Aprili 2013 kuhusu bidhaa wanazotengeneza aina ya BATIKI na changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo ufinyu wa mtaji wa kikundi ili kuweza kuzalisha aina mbalimbali za BATIKI na kushiriki katika maonyesho ya kimataifa ya kibiashara. Kikundi cha Faith ni moja kati ya vikundi vya Kijamii na Vyama vya Ushirika mjini Kyela vinavyonufaika na mradi wa UKIMWI na uwezeshaji wa Kiuchumi unaoratibiwa na ILO.
Katibu wa Kikundi cha Mshikamano wajasiriamali mjini Kyela mkoani Mbeya Bw. Nazar Mwaipasi akifafanua kuhusu maendeleo ya kikundi ikiwa ni pamoja na kuanzisha SACCOS punde baada ya kutembelewa na Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania mnamo tahere 2 Aprili 2013.Bw. Nazar aliongeza kuwa kikundi cha Mshikamano kinachoundwa na wanawake na vijana wa kike na kiume wanaojihusisha na biashara binafsi na usindikaji wa vyakula kama mafuta ya mawese, samaki, mapishi na biashara ya mchele, kiliundwa baada ya mafunzo ya ujasiriamali na UKIMWI yaliyotolewa kwa wanawake na vijana kupitia mradi wa UKIMWI na uwezeshaji wa Kiuchumi wa ILO.



































