Wananchi waliofurika katika Tamasha la Filamu la Grand Malt linalofanyika katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza wakifuatilia mambo yanavyoendelea.
********************************
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MWANZO MWISHO! Leo ni leo katika Uwanja wa Nyamagana jijini hapa, wakati kutakapofungwa rasmi Tamasha la Wazi la Filamu la Grand Malt Tanzania, maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ lililokuwa likifanyika kwa wiki nzima.
Huku wasanii wote mashuhuri wa filamu wakitarajiwa pia kufanya vitu vyao jukwaani, kazi kubwa itakuwa kwa burudani kali zitakazotolewa wakati wa kufunga tamasha hilo.
Mbali na hilo, pia kutakuwa na shindano kali hatua ya fainali ya kusaka wakali wa kurap pamoja na kukata nyonga, ambao nao watajiondokea na kitita kikubwa cha fedha.
Akizungumzia hilo, Mratibu wa Tamasha hilo, Musa Kissoky, alisema kutakuwa na mambo makubwa zaidi uwanjani hapo na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia kile kitakachoendelea.
“Kila kitu kipo tayari na wasanii wote wakali wa filamu watakuwepo ili kutoa burudani kwa mashabiki waliofika hapa, huku kukiwa na filamu mbalimbali zitakazooneshwa,” alisema.
Baadhi ya wasanii wa filamu wanaotarajiwa kuwepo ni Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Vicent Kigosi ‘Ray’, Shamsa Ford, Ritchie Ritchie, Steven Jacob ‘JB’, Chuchu Hans, Steve Nyerere, Hashim Kambi na wengineo wengi.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam alisema, amefurahi kuona tamasha hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa, huku akitaka mashabiki kufurika Nyamagana leo kuona kile kinachoendelea.
“Hapa Mwanza tumeshuhudia vipaji vya kila aina, nimefurahi kwa kiasi kikubwa kuona mashabiki walivyolipokea tamasha hili, kwetu Grand Malt tunaamini lengo letu limefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Katika mashindano ya kurap na kucheza katika kila eneo mshindi wa kwanza anatarajiwa kuondoka na Sh 200,000 wa pili Sh 100,000 na watatu Sh 50,000.
Tamasha la Filamu la Grand Malt lilianza rasmi mwishoni mwa wiki na linatarajiwa kumalizika leo, huku wakati wote wa tamasha hilo zikionyeshwa filamu mbalimbali za Tanzania.
Tamasha hilo la filamu limedhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi ambacho kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)
No comments:
Post a Comment