Tuesday, May 21, 2013

*TIMU 14 RCL KUUMANA RAUNDI YA PILI WIKIENDI



Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao inaingia raundi ya pili wikiendi hii kwa kukutanisha timu 14 zilizofanikiwa kusonga mbele.

Timu zitakazocheza raundi hiyo kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ni Abajalo ya Dar es Salaam itakayokuwa mwenyeji Kariakoo ya Lindi katika mechi itakayochezwa Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Siku hiyo hiyo Uwanja wa Azam ulioko Chamazi utatumika kwa mechi kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga wakati Jumapili (Mei 26 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Machava FC ya Kilimanjaro na Mpwapwa Stars ya Dodoma itakayochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Stand United ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida katika mechi itakayochezwa Jumapili (Mei 26 mwaka huu) Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati Polisi Jamii ya Mara na Biharamulo FC ya Kagera zitaumana siku hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Mjini Kigoma kutakuwa na mechi kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi. Nayo Kimondo SC ya Mbeya itakuwa mgeni wa Njombe Mji ya Njombe katika mechi itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sabasaba.

Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu wakati timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment