Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la mustakabali wa mtoto wa kike katika mazingira ya sasa litakalofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Hayo yalisemwa leo mjini Dodoma na Katibu wa Taaluma wa Umoja wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Jasmine Mtua wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo.
“ Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na vyuo vingine umeandaa kongamano hili,” alisema Jasmine.
Jasmine aliongeza kuwa Mama Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ataambatana na baadhi ya waziri na wabunge wanawake.
Alisema kauli mbiu katika kongamano hilo ni “Wanawake tukithubutu tunaweza”.
Aliongeza kuwa mada zitakazo jadiliwa katika kongamano hilo ni jinsi ya kuwa kiongozi, afya ya uzazi, malengo ya kujitambua, nafasi ya mtoto wa kike katika Katiba mpya .
Vyuo vitakavyoshiriki kwenye Kongamano hilo ni Chuo cha Biashara(CBE), Chuo Kikuu cha St. John,Chuo cha Serikali za Mitaa(Hombolo) Chuo cha Madinina na Dodoma sekondari.
mwisho.
No comments:
Post a Comment