Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George Yambesi (kulia) na Afisa Masoko na Mauzo TTCL Bw. Peter Ngota (kushoto) wakitia saini mkataba wa makubaliano ya kuweka mtandao mmoja wa mawasiliano Serikalini hivi karibuni jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George Yambesi (kulia) akibadilishana Mkataba waliosaini Mkurugenzi wa Kampuni ya Softnet Gilbert Herman (kushoto)hivi karibuni jijini Dar es salaam .
Mtendaji Mkuu Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Bakari (kushoto) akiwapongeza makampuni ya Kitanzania ya TTCL na Sosftnet kwa kushinda zabuni ya kujenga mtandao wa mawasiliano na kuyashinda kampuni nyingine duniani. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George Yambesi.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria hafla ya kusaini mikataba ya kuweka Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali kati ya hivi karibuni jijini Dar es salaam. Picha zote na Eliuteri Mangi-Maelezo
********************************
Na Eleuteri Mangi-Maelezo
Serikali imetiliana saini makubaliano na makampuni yaliyoshinda zabuni ya kujenga mtandao wa mawasiliano.
Makubaliano hayo yalisainiwa hivi karibuni jijini Dar es salaam kati ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George Yambesi kwa niaba ya Serikali na kampuni ya Softnet Teknology Ltd pamoja na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Katibu Mkuu Yambesi alisema kuwa mradi huo unalenga kuweka mtandao mmoja wa mawasiliano Serikalini na taasisi zake na unasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma (OR-MUU).
“Mradi huu ni hatua muhimu ya utekelezaji wa Serikali Mtandao ukiwa na lengo la kuipatia Serikali na taasisi zake mawasiliano ya sauti, data, nyaraka na picha yenye uhakika, rahisi, salama na yanayopatikana kwa muda wote” alisema Katibu Mkuu Yambesi.
Akifafanua kuhusu malengo ya mradi huo Yambesi amesema yanaenda sanjari na malengo ya kujengwa kwa mkongo wa Taifa na utekelezaji wa sera ya Serikali mtandao, Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003, programu ya mabadiliko ya utekelezaji wa kazi na utoaji wa huduma katika katika Utumishi wa Umma.
Malengo mengine ni Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini (MKUKUTA), Mpango Taifa wa Maendeleo ya miaka mitano 2012 hadi 2016 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Katibu Mkuu Yambesi alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utazihusu Wizara, Idara zinazijitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikakali za Mitaa.
Aidha, mkataba huo utazihusisha taasisi 72 ambazo ni Wizara zote, Idara zinazojitegemea 16 na Wakala 30 zitaunganishwa kwenye mtandao huo.
Katibu Mkuu Yambesi alisisitiza kuwa taasisi zilizobaki zikiwemo Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na Idara nyingine za Serikali zitaunganishwa kwenye mtandao huo kwa kutegemea upatikanaji wa fedha.
Naye Mtendaji Mkuu Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Bakari alisema kuwa amefarijika na ushindi wa makampuni ya Kitanzania yaliyoshinda tenda ya kutekeleza mradi huo mara baada ya kuzishinda kampuni nyingine duniani.
Dkt. Jabiri Bakari aliongeza kuwa mradi huo utaongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa sekta ya Umma ambapo kutakuwa na mawasiliano rahisi, imara na uhakika baina yake na wadau wote nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Softnet Nuru Othman aliishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi hiyo na ametoa wito kwa Makampuni ya Kitanzania watumie uwezo wao kufanya kazi kwa weledi ili kufanya makampuni ya Kitanzania yatambuliwe na kuaminika Kimataifa.
Mradi huu unafadhiliwa na Benki kuu ya Dunia kuptia programu ya miundimbinu ya “Reginal Communication Infrastructure Program- (RCIP) Tanzania”
No comments:
Post a Comment