Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Lameck Nchemba
Serikali imeliagiza Bunge Maalumu la Katiba na taasisi za fedha kutowaingizia fedha wajumbe wa Bunge hilo waliojitoa juzi kwenye mchakato wa katiba.
Agizo hilo lilitolewa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge hilo.
“Niliagiza kuwa fedha hizo zitakapotoka Bunge zinatakiwa kupelekwa kwenye mabenki…na zilishakamilika kwa Bunge, lakini zilikuwa bado hazijakamilika kwa mujibu wa benki kuzipeleka kwenye akaunti za wajumbe,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwigulu, aliziagiza taasisi hizo za fedha kufuta uhamisho wa fedha za wajumbe, ambazo hazijakamilika na hakuna mjumbe yeyote, ambaye ametoka nje kupewa fedha hadi hapo watakaporudi bungeni Aprili 22, mwaka huu.
Alisema wajumbe wanatakiwa kulipwa fedha kulingana na watakavyokuwa wanaingia kwenye vikao na wale ambao hawataingia hawatapewa fedha.
“Hakuna mtu kuchukua fedha na kwenda kufanyia sherehe ya sikukuu wakati kuna watu, ambao wana shida kubwa sana na hawajapata fedha hizi kwa sababu tumepeleka kipaumbele kwenye mchakato wa katiba,” alisema.
Alisema kuna watu wanafanya kazi kwenye halmashauri mbalimbali na wanaidai serikali kutokana na kazi zao halali walizofanya, lakini hawajalipwa fedha zao kwa ajili ya ufinyu wa bajeti, huku wakipewa wajumbe kwa kuweka kipaumbele cha katiba.
No comments:
Post a Comment