Friday, April 18, 2014

VIJANA WATAKIWA KUJIUNGA NA VIKUNDI VYA UJASILIAMALI ILI WAMUDU KUJUKWAMUA KIMAISHA



Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Vijana mkoani Lindi wametakiwa kuacha tabia ya kuilalamika Serikali kuwa maisha ni magumu bali watumie  fursa zilizopo katika maeneo yao kwa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kujiajiri na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha. 

Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Baraza kuu na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCC) taifa kutoka mkoa wa Lindi Jabiri Makame kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha   Mnazi mmoja wilaya ya Lindi Mjini kwa ajili ya kuzipokea mbio za kizalendo za pikipiki na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Jabiri alisema  vijana wengi wamekuwa wakiilalamika Serikali kutokana na changamoto zinazowakabili na kusahau kuwa kazi ya Serikali ni hakikisha kwamba inawaandalia mazingira mazuri ya wao kuweza kujikwamua kiuchumi  na kuweza kujiletea maendeleo hii ni pamoja na kuwapatia mikopo.

“Halmashauri zetu zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kinamama na vijana naamini hata Halmashauri za mkoa huu zinafanya hivyo lakini fedha hizo hazitolewi kiholela ni lazima wahusika wajiunge  katika makundi yaliyosajiliwa  kwa mfano  kundi la madereva wa bodaboda, bajaji, kina mama lishe na vikundi vya mpira pia vinaweza kuwa vya ujasiriamali na kuweza kupata mkopo ambao watautumia katika shughuli zao za maendeleo”, alisema Jabiri.

Kuhusu suala la uongozi alisema Rais Kikwete anawaamini sana vijana na ndiyo maana amewateua na kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama na Serikali na kutoa mfano wa mawaziri na wakuu wa wilaya.  
Jabiri alisisistiza, “Katika uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa  na Uchaguzi mkuu mwakani vijana wa CCM msiogope kuomba nafasi za uongozi  wakati ukifika wajitokeze kuchukuwa fursa za uongozi jambo la muhimu ni kutotangaza  nia mapema subirini hadi wakati utakapofika”.

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo aliwapongeza UVCCM kwa kuandaa mbio hizo za uzalendo kwani ni ukweli usiopingika kuwa Muungano wenye dhana ya kizalendo na historia ya nchi unatimiza miaka 50 tarehe 26/4/2014.

Mama Kikwete alisema, “Leo hii nchi kubwa zenye nguvu kiuchumi Duniani zinazungumzia suala la kuungana ili kuimarisha nguvu yao ya pamoja , kwanini sisi tukubali kutengana? Muungano wetu ni kigezo kizuri ndani ya Bara la Afrika  na kote Duniani tusikubali kamwe kuuvunja jambo kubwa hapa na la msingi ni kukaa kwa pamoja na kujadili hatimaye kupata ufumbuzi yakinifu”. 

MNEC huyo alisema vijana wa CCM ndiyo wanaotegemewa kuwa viongozi hapo baadaye, walipoona kuna watu wanataka kupotosha ukweli juu ya umuhimu na faida za kuwa na muundo wa Serikali mbili wakaamua kuzunguka nchi nzima na kuunga mkono umuhimu wa nchi kuwa na Serikali mbili na siyo moja wala tatu kama vinavyotaka vyama vingine vya Siasa. 

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi Mzee Ally  Mtopa alisema Mwenyezi Mungu amemuumba binadamu katika umbo la mapenzi na  kumpa akili ya kuweza kuchagua lipi alifuate kati ya jema na baya hivyo ni muhimu kwao kuweza kuamua ni chama gani cha kuweza kuingia na siyo kukurupuka.

“Sisi wanachama wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Lindi na Tanzania nzima tunaunga mkono muundo wa Serikali mbili na kuwepo kwa muungano ambao umetuletea manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na watu kutoka Tanzania bara na Visiwani kuishi pamoja kwa amani na upendo”, alisema Mzee Mtopa.

UVCC mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara waliandaa mbio za uzalendo za pikipiki zenye kauli mbiu Miaka 50 ya Muungano Dumisha Muungano, vijana tutumie fursa zilizopo katika maeneo yetu. Tanzania kwanza mengine baadaye ambazo zilizinduliwa mkoani Ruvuma katika wilaya ya Namtumbo tarehe 13/4/2014 kumalizika mkoani Lindi tarehe 17/4/2014.

Mkoa wa Lindi ulizipokea mbio hizo kutoka kwa UVCCM mkoa wa Mtwara makabidhiano yaliyofanyika kata ya Madangwa na katika mkutano wa hadhara uliofanyika hapo jumla ya wanachama watatu walijiunga na Chama hicho wawili kutoka chama cha Civic United Front (CUF) na mmoja kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) .

Lengo la mbio hizo ni kuwaenzi waaasisi wa Taifa la Tanzania  ambao ni Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuwafikishia ujumbe watanzania  juu ya umuhimu wa muungano na kuwaeleza wapi ulipotoka, ulipo na unakokwenda na vijana kutumia fursa zilizopo kujiedeleza.

Katika mkutano huo jumla ya wanachama wapya vijana 19 walijiunga na umoja huo, mmoja alirudisha  kadi ya uanachama wa CHADEMA na kujiunga na chama hicho.

No comments:

Post a Comment