Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu WA Mtaa wa Mwanakwerekwe wakiwa ndani ya Msikiti Muhammad { SAW } wakishuhudia tendo la kukabidhiwa msikiti huo uliokua umefungwa karibu miaka 14 kutokana na hitilafu ya mgongano wa umiliki wa matumizi yake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mwanakwerekwe kabla ya kukabidhi rasmi hati ya umiliki wa matumizi wa msikiti Muhammad { SAW } kwa waumini hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikabidhi rasmi hati ya umiliki wa matumizi wa msikiti Muhammad { SAW } kwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana hapo uliopo msikiti huo Mtaa wa Mwanakwerekwe.
Katibu Mtendaji wa Wakfu na Malio ya Amana Zanzibar Sheikh Abdulla Talib akimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa Uamuzi wa Serikali kuruhusu msikiti Muhammad { SAW } uendelea kufanyiwa ibada.
Kati kati ni makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na wakwanza kushoto ni Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Kabi.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhi rasmi hati ya umiliki wa matumizi ya Msikiti Muhammad { SAW } uliopo nyuma ya Tawi la Benki ya Kiislamu ya Watu wa Zanzibar {PBZ } uliopo Mwanakwerekwe kwa waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa huo ili waendelee kuutumia katika Ibada zao mbali mbali za kila siku.
Msikiti huo ulikuwa umefungwa kutumika kwa suala lolote la ibada kwa karibu miaka 14 sasa tokea miaka ya 2000 baada ya kutokea hitilafu ya umiliki wa msikiti huo baina ya waumini wa dini hiyo waliokuwa wakiutumia kwa ibada zao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi hati hiyo kwa waumini hao kupitia kwa Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Sheikh Abdulla Talib na Baadaye Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Kabi ambapo amesema waislamu wasingependa kuona msikiti huo unaharibiwa bila ya kutumika.
Balozi Seif alisema imesikitisha kuona baadhi ya watu walikuwa wakifanya uchafu ndani ya msikiti huo kwa muda mrefu wakati taratibu na sheria za kiislamu kamwe haziruhusu hata kuingia na viatu ndani ya nyumba hiyo ya ibada.
Alieleza kwamba Serikali ilifikia uwamuzi wa kuukabidhi msikiti huo kwa waumini wa eneo hilo kufuatia vikao mbali mbali ikiwemo mahkama ya rufaa Tanzania iliyoamua kufuta amri zote zilizohusika na msikiti huo.
“ Vikao mbali mbali vilivyohusu suala la msikiti huo vilifikia uamuzi wa msikiti huo kutumiwa tena na waumini kutekeleza ibada zao za kila siku “. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa wa Mwanakwerekwe mmoja wa Wazee wa Mtaa huo Sheikh Mwinshehe Othman ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu wataisimamia katika masuala ya ibada na si vyenginevyo.
Hata hivyo Sheikh Mwinshere aliiomba Serikali kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuiangalia bara bara ya kuingia kwenye msikiti huo kutokea bara bara kuu ya mwanakwerekwe ambayo haipitiki kutokana na uchafuzi wa mazingira.
Alisema ni vyema katika kuunga mkono nguvu za Waumini hao katika kuurejeshea hadhi yake msikiti huo Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi au Baraza la Manispaa likaweka nguvu zake katika kuifanyia marekebisho bara bara hiyo ili kutoa fursa kwa waumini pamoja na wananchi kuitumia bila ya usumbufu wowote.
Kamisheni ya Ardhi na Mazingira Zanzibar Tarehe 16 Agosti mwaka 1991 ilitoa hati umiliki wa ardhi ya eneo hilo kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti, Chuo pamoja na Kituo cha Afya yenye kumbu kumbu namba MU/21 – Kiwanja D6 kikiwa na ukubwa wa Square Metre Mia 330.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment