Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Sweeden Balozi Dora Msechu wa pili kutoka kushoto aliyevaa nguo rangi ya njano akiaga rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baada ya
kuchanguliwa kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimuomba Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Sweeden Balozi Dora kuitanga sera ya Utalii Zanzibar kwenye taasisi na mashirika ya kigeni awapo kwenye utumishi wake Nchini Sweeden.
Mazungmzo hayo yalifanyika ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Ofisi za Kibalozi za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zimekumbushwa kuendelea kuitangaza Sera ya Utalii iliyoanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mpango wake wa kuimarisha uchumi ili kuacha tegemezi la zao moja la karafuu ambalo baadhi ya wakati hupata changamoto inayosababisha kutetereka kwa mapato ya Taifa.
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Sweeden Mh. Dora Msechu aliyefika kumuaga akijiandaa kwenda kutekeleza kazi yake mpya aliyokabidhiwa na Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimtaka Balozi Dora kuitangaza vyema Zanzibar Kiutalii wakati zinapotokea fursa za uwekezaji kwenye mataifa anayokwenda kufanya kazi akiiwakilisha Tanzania.
Alieleza kwamba Zanzibar hivi sasa inategemea zaidi Diplomasia ya kiuchumi katika kuimarisha mipango yake ya maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii kwa kushirikiana na Mashirika, Taasisi na Mataifa mbali mbali rafiki na hisani.
“ Wewe ndie sikio letu, Wewe ndie mwakilishi wetu kwenye eneo la kidiplomasia katika kutetea maslahi ya Taifa “. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtanabahisha Balozi Dora.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na uteuzi aliyopata Balozi Dora Msechu ambae si mgeni katika shughuli mbali mbali za Kidiplomasia alizozianza mwanzoni mwa ajira yake.
Alimuomba Balozi huyo Mteule wa Tanzania Nchini Sweeden kuwasiliana na taasisi zinazosimamia sekta ya utalii ili kupata vielelezo vya kina vinavyofafanua hali halisi ya mazingira na vivutio vya uwekezaji katika sekta ya Utalii hapa Zanzibar.
Mapema Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Sweeden Mh. Dora Msechu alisema heshima aliyopewa na Taifa imempa faraja kubwa iliyotowa fursa kwake kujiandaa kufanya kazi kwa nguvu zake zote.
Balozi Dora alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba muda wote yuko tayari kupokea agizo, mawazo na busara za waliomtangulia katika utumishi wa umma ili atekeleze kazi zake kwa kujiamini.
Akigusia sekta ya Utalii iliyopewa nafasi kubwa ya kuchangia uchumi wa Zanzibar Balozi Dora Msechu aliitanabahisha Serikali pamoja na viongozi wanaosimamia sekta hiyo kuhakikisha kwamba suala la amani na usalama wa wawekezaji ndio jambo la msingi katika utekelezaji wa sera hiyo.
Balozi Dora alisema ukosefu wa mambo hayo mawili muhimu ni kusema kwamba kasi na nguvu za Serikali katika kuimarisha sekta hiyo inaweza ikawa ya bure na kupoteza nguvu na fedha nyingi bure.
Othm,an Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/5/2014.
No comments:
Post a Comment