Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shen akikata utepe kuashiria kukifungua rasmi Kituo cha Afya cha Mama na Watoto katika Kijiji cha Bwejuu Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif akiangalia aadhi ya Vitanda vitakavyotumiwa na Watoto watakaozaliwa katika Kituo cha Afya cha Mama na Watoto cha Kijiji cha Bwejuu mara tuu baada ya kukifungua rasmi.
Vijana wa Sarakasi wa Kijiji cha Muungoni wakitoa burdani ya aina yajke kwenye hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Afya cha Mama na Watoto cha Kijiji cha Bwejuu Wilaya ya Kusini.
Mkurugenzi wa Hoteli ya Zanzibar Collection Breeze Bwana Adriano Fusillo akiwapongeza wananchi wa Bwejuu kwa ushirikiano na wafanyakazi wa hoteli yake kwenye hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Afya cha Bwejuu.
Mwakilishi wa Taasisi ya misaada ya Afya ya Kimataifa ya New Hope Sweeden Bwana Jackob Moiwawa akiwasilisha salamu za Taasisi hiyo kwenye hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Afya cha mama na watoto Bwejuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Bwejuu mara baada ya kukifungua Kituo cha afya cha Kijiji hicho kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Sheni.
Mandhari ya nje ya Kituo cha Afya cha huduma za Mama na Watoto cha Kijiji cha Bwejuu kilichofunguliwa rasmi kutoa huduma na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Sheni.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuyapongeza mashirika na Taasisi mbali mbali za maendeleo ndani na nje ya Nchi kwa juhudi wanayochukuwa katika kusaidia maendeleo ya Wananchi hasa sekta ya afya ambayo ni muhimu katika ustawi wa Jamii.
Juhudi hizo zimeisaidia sana Zanzibar katika harakati zake za kuimarisha sekta ya afya na kufikia lengo la millennia la kuwa na huduma za afya masafa ya kila baada ya kilomita Tano.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Sheni wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa Kituo cha Afya cha huduma za Mama na Watoto katika Kijiji cha Bwejuu Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif alisema Visiwa vya Unguja na Pemba hivi sasa vimefanikiwa kuwa na Vituo vya Afya vipatavyo 134 ikiwa ni mafanikio makubwa kupindukia lengo la millennia wakati kabla ya Mapinduzi Zanzibar nzima ilikuwa na Vituo vya Afya 32 vya Serikali pamoja na Viwili Binafsi.
Aliwahakikishia wananchi kwamba Vituo vitakavyoendelea kujengwa sehemu mbali mbali Mjini na Vijijini vitatoa huduma inayostahiki kwa vile Serikali tayari imeshajipanga kusomesha Madaktari na wauguzi ili kukidhi mahitaji halisi ya Hospitali na Vituo vya Afya hapa Nchini.
“ Wananchi wasiwe na wasi wasi Serikali itaendelea kujitahidi kusomesha madaktari na wauguzi ili kuondosha upungufu wa watendaji wa afya katika baadhi ya Hospitali na Vituo vya afya kwenye maeneo yetu “. Alieleza Balozi Seif.
Alisisitiza kwamba licha ya ujenzi wa vituo vingi vipya vya Afya katika maeneo mbali mbali Nchini lakini Serikali pia imefanya juhudi kubwa ya kuvifanyia matengenezo makubwa Haospitali na baadhi ya vituo vya afya vya zamani ili kutoa huduma sambamba na vile vipya vilivyoanzishwa.
Balozi Seif aliwakumbusha wananchi kwamba miradi ya kijamii lazima ianzishwe na kusimamiwa na wao wenyewe ili Serikali pamoja na Wafadhili wapate fursa na ushawishi wa kuunga mkono miradi hiyo.
Aliwapongeza wananchi wa Kijiji cha Bwejuu kwa bahati waliyoipata na kuitumia vyema katika kuanzisha miradi yao ya kiuchumi na ustawi wa jamii huku wakiungwa mkono na wafadhili hasa wale wawekezaji waliomo ndani ya maeneo yao.
Alisema wapo Wananchi wengine katika baadhi ya maeneo Mijini na vijijini hufanikiwa kupata fursa kama hizo lakini wakashindwa kuzitumia ipasavyo kwa sababu za kushawishiwa kisiasa.
Akisoma Risala ya Wananchi hao wa Bwejuu Diwani wa Wadi ya Bwejuu Ndugu Juma Mussa Mkali alisema Kamati ya Afya ya Kijiji hicho ilifikia uamuzi wa Kujenga kituo cha Afya kufuatia mji wa Kijiji hicho kukumbwa na wimbi kubwa la watu kutokana na ongezeko kubwa la uwekezaji wa Hoteli za Kitalii.
Diwani Juma alitoa pongezi kwa Uongozi wa Hoteli za Kitalii za Breeze, Baraza, Palm pamoja na Taasisi ya Kimataifa ya Misaada ya Afya ya New Hope ya Nchini Sweeden kwa uwamuzi wao wa kufadhili ujenzi wa Kituo hicho kitakachokuwa mkombozi kwa akina mama na Watoto.
Hata hivyo Nd. Juma alisema bado Kituo hicho kinakabiliwa na baadhi ya changamoto akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na Hati miliki ya jengo, uzio pamoja na nyuma za wafanyakazi.
Akitoa salamu za Taasisi ya Misaada ya Afya ya Kimataifa ya New Hope Sweeden ikiwa ni miongoni mwa wafadhili wa ujenzi wa Kituo hicho cha afya cha Bwejuu Mwakilishi wake hapa Zanzibar Bwana Jackob Moiwawa alisema Taasisi hiyo imefarajika kuona huduma za afya za akina mama na watoto katika Kijiji hicho zitapatikana katika kiwango kinachokubalika.
Bwana Moiwawa alisema New Hope Sweeden iliyoanzishwa karibu miaka 25 iliyopita ina lengo la kutoa huduma za afya popote pale ulimwenguni kutegemea mahitaji ya nchi na wananchi wanaohusika.
“ New Hope Sweeden chini ya muanzilishi wake Bibi Ragus inafuraha kuona inasaidia huduma za afya za akina mama na watoto katika kijiji cha Bwejuu ikielewa kwamba kila wakati watoto wanazaliwa na kuhitaji matunzo na afya njema “. Alisema Mwakilishi huyo wa New Hope Sweeden.
Naye Mkurugenzi wa Zanzibar Collection Breeze ambayo nayo pia mshirika wa ujenzi wa Kituo hicho cha Afya Bwana Adriano Fusillo alisema watoto wanahitaji mwanzo mzuri wa maisha yao kwa kupata huduma bora za afya ya msingi.
Bwana Adriano aliwahakikishia Wanakijiji wa Bwejuu kwamba Uongozi wa Hoteli yake utaendelea kuwaunganisha wananchi hao katika kusaidia huduma za afya, maendeleo pamoja na Utamaduni.
“ Ahsanteni sana watu wa Zanzibar kwa kutukubalia sisi wageni kuishi na kutafuta maisha hapa Zanzibar kitendo ambacho kimetupa faraja na kufikia hatua na moyo wa kusaidia kwa hali na mali harakati za Kiuchumi na ustawi wa jamii “. Alielezea faraja yake Bwana Adriano.
Mapema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Jamala Adam alisema Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja imeonyesha kuwa na viashiria vizuri vya huduma za afya hasa zile huduma za akina mama na Watoto.
Dr. Jamala alifahamisha kwamba vifo vya akina mama na watoto vimepungua kiasi katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Zanzibar takwimu zikionyesha kuwa vifo vya akina mama vilipungua na kufikia 275 kati ya 100,000 mwaka 2012.
Alisema lengo la Wizara ya Afya Zanzibar ifikapo mwaka 2015 ni kupunguza zaidi vifo vya akina mama vifikie 170 kwa kila wanawake 100,000 na kudhibiti vifo vya watoto vifikie 50 kwa kila watoto 1,000.
Hoteli sita kati ya 25 zilizopo kwenye ukanda wa Kijiji cha Bwejuu zilikubali kusaidia ujenzi wa kituo hicho cha Afya miongoni mwake ni pamoja na Breeze Hoteli, Baraza, Palm pamoja na Taasisi ya Misaada ya Afya ya Kimataifa ya New Hope Sweeden.
Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya cha Bwejuu ulioanza Tarehe 23 mwezi Febuary mwaka 2008 kupitia Jumuiya ya Mazingira ya Jozani uligharimu jumla ya Shilingi Milioni Mia Mbili na Tano { 205,000,000/- } mchango wa wahisani ukafikia shilingi Milioni 192,700,000/-.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/5/2014.
No comments:
Post a Comment