Usajili wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2014/2015) unaanza Juni 15 hadi Agosti 3 mwaka huu wakati kipindi cha kutangaza wachezaji walioachwa au kusitishiwa mikataba ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu.
Kipindi cha kwanza cha uhamisho wa wachezaji ni kuanzia Juni 15 mwaka huu hadi Julai 30 mwaka huu. Kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Agosti 4 na 11 mwaka huu. Kuthibitisha usajili hatua ya awali ni Agosti 12 hadi 14 mwaka huu.
Usajili hatua ya pili utakuwa kati ya Agosti 14 na 29 mwaka huu. Kupitia na kutangaza majina ya pingamizi hatua ya pili ya usajili ni kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4 mwaka huu. Uthibitisho wa usajili hatua ya pili ni Septemba 5 na 6 mwaka huu.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu, na ratiba inatarajiwa kutoka mwezi mmoja kabla (Julai 24 mwaka huu).
*MECHI YA TAIFA STARS YAINGIZA MIL 63/-
Mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe iliyochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 63,345,000.
Mapato hayo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 yametokana na washabiki 11,079 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000.
Mgawo wa mapato hayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 9,662,796.61, gharama za kuchapa tiketi sh. 6,000,000, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 7,152,330.51, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 9,536,440.68 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa pamoja wamepata sh. 30,993,432.20.
*MASHABIKI WA SOKA KWENDA HARARE KUSHANGILIA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaandaa utaratibu utakaowawezesha washabiki kwenda jijini Harare, Zimbabwe kushuhudia mechi ya Taifa Stars.
Mechi hiyo ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa ajili ya fainali zitakazochezwa Morocco mwakani itafanyika Jumapili (Juni 1 mwaka huu) jijini Harare.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.
Usafiri huo utakuwa wa basi ambapo washabiki wanatarajiwa kuondoka siku ya Ijumaa na kuwasili Jumapili mchana jijini Harare ambapo watashuhudia mechi na kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo.
Washabiki wanatakiwa kuwa na hati za kusafiria (pasipoti), nauli ya kwenda na kurudi itakuwa sh. 300,000.
*TIMU YA U15 YAWASILI GABORONE
Timu ya Tanzania ya umri chini ya miaka 15 imewasili salama jijini Gaborone, Botswana kwa ajili ya michezo ya Afrika ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Mei 22 mwaka huu dhidi ya Mali.
Kikosi hicho cha wachezaji 16 chini ya Kocha Abel Mtweve kimetua jijini Gaborone jana (Mei 19 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South African Airways. Michezo hiyo itamalizika Mei 30 mwaka huu.
Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Tanzania ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.
Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland.
Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambazo nazo zilikuwa zishiriki kwenye michezo hiyo katika dakika za mwisho.
*NGORONGORO HEROES YAENDA NIGERIA
Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) chenye watu 25 kinaondoka kesho alfajiri kwenda Nigeria kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).
Mechi hiyo itachezwa Jumamosi (Mei 24 mwaka huu) katika Jiji la Kaduna kwenye Jimbo la Kaduna ambalo lipo katikati ya Nigeria.
Msafara wa timu hiyo unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi unaondoka kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
Msafara wa timu hiyo unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi unaondoka kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
Ngorongoro Heroes inayonolewa na Kocha John Simkoko ilipoteza mechi ya kwanza iliyofanyika nyumbani jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0.
Mwamuzi Alhadi Allaou Mahamat wa Tchad ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Atasaidiwa na Issa Yaya, Alfred Madjihoudel na Idriss Biani wote kutoka Tchad. Kamishna ni Aboubakar Alim Konate wa Cameroon.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment