TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 16, 2014
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo anawafahamu wachezaji wengi.
Amesema wachezaji wanaounda kikosi chake ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Nooij amesema ujio wa washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.
Samata na Ulimwengu watawasili nchini Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.
Wachezaji waliopo kambini kwa sasa ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin Friday.
Wakati huo huo, timu ya Zimbabwe (Mighty Warriors) inawasili kesho alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 27. Kesho saa 4 asubuhi (Mei 17 mwaka huu) Kocha wa timu hiyo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zinaanza kuuzwa kesho (Mei 17 mwaka huu) kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, OilCom Ubungo, Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala. Viingilio ni sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 tu.
…MDAU AAHIDI WACHEZAJI MIL 5/-
Mdau mmoja wa mpira wa miguu ambaye hataki jina lake litajwe ameahidi kutoa sh. milioni tano kwa wachezaji wa Taifa Stars iwapo wataifunga Zimbabwe katika mechi ya Jumapili.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linamshukuru mdau huyo, na linatoa mwito kwa wadau wengine wajitokeze kutoa motisha kwa Taifa Stars.
Bonasi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa wachezaji wa Taifa Stars itatolewa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
No comments:
Post a Comment