Sunday, May 18, 2014

USHIRIKIANO WA PAMOJA UNAHITAJIKA ILI KUJENGA NIDHAMU YA MWANAFUNZI.ASEMA MAMA SALMA KIKWETE



Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari ya mama salma
Ushirikiano wa pamoja unatakiwa baina ya wanafunzi, walezi, wazazi, jamii na walimu ili kuweza kujenga, kuimarisha na kukuza nidhamu , mwenendo na tabia ya mtoto jambo ambalo litaleta mafanikio chanya pamoja na kutatua changamoto za kitaaluma na kimazingira.

Hayo yamesemwa  jana  na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na walimu pamoja  na wanafunzi wa shule ya Sekondari  Salma Kikwete iliyopo kata ya Kijitonyama wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema nidhamu ya mwanafunzi siyo tu kumuamkia mwalimu bali pia kujua wajibu wake kama vile kuwahi shuleni, kufanya mazoezi ya darasani na kusoma kwa bidii.

“Neno nidhamu lina dhana pana kwani linagusa wengi lakini katika mazingira ya leo walengwa wakubwa ni  mzazi,mlezi au jamii, mwalimu na mwanafunzi. Kazi ya mzazi, mlezi na jamii ni kuhimiza na  kufuatilia maendeleo ya mtoto.

Mwalimu kufundisha, kuingia darasani kwa wakati  na kujiandaa  na kwa mwanafunzi ni kupokea maarifa anayopewa na mwalimu wake na kusoma kwa bidii”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wa wanafunzi aliwasihi kuongeza juhudi katika masomo na kufanya vizuri kwenye mitihani,  kwani wao na wengine wote wanategemewa na familia, jamii zao na taifa kwa kuwa watakuwa wakombozi siku za  baadaye na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na ujasiri katika safari yao ndefu ya kufatuta elimu.

Aidha Mama Kikwete aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya uboreshaji wa elimu pamoja na kukabiliwa na changamoto kadhaa lakini kadri siku zinavyokwenda mbele ndivyo Serikali inavyozidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowahusu walimu.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisisitiza,  “Walimu timizeni wajibu wenu  kwa kufika kazini mapema, kumaliza silabasi kwa wakati, kukamilisha maandalio ya masomo, kufundisha kila kipindi bila kukosa, kujua taarifa na udhaifu wa wanafunzi wenu na kuwa kiungo kati yenu  na wazazi au walezi hiyo  ndiyo nidhamu ya mwalimu na ndiyo ualimu”.

Akisoma taarifa ya shule hiyo Mwalimu Elestina Chanafi alisema shule hiyo ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 320, walimu 13 na vyumba vya madarasa sita hivi sasa ina wanafunzi 1229, walimu 33 na  vyumba vya madarasa 22. Hadi sasa jumla ya wanafunzi 1161 wamehitimu masomo yao tangu walipoanza  kutoa kidato cha nne mwaka 2010. 

Mwalimu Chanafi  ambaye ni Mkuu wa shule hiyo alisema wamefanikiwa kuchimba kisima cha maji kwa msaada wa wakorea, kuunganisha umeme, kununua vifaa mbalimbali vya uchapaji na udurushaji, kuboresha mazingira kwa kiwango cha kutia moyo na kuweza  kuwavutia wanafunzi ili wajisikie kuwa sehemu ya shule.

Kuanzisha maabara ya muda ambayo imewawezesha wanafunzi wa sayansi kufanya mitihani kwa vitendo na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo na kupata wanafunzi wa kujiunga na masomo ya ngazi ya juu kwa idadi nzuri.

“Changamoto zinazotukabili ni uchakavu wa baadhi ya vyumba vya madarasa, mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao unasababisha ugumu katika kudhibiti nidhamu ya wanafunzi, uelewa mdogo wa wazazi juu ya mchango wao kwa maendeleo ya wanafunzi, kiwango kidogo cha ruzuku toka Serikalini ambacho hakiletwi kwa ukamilifu na wakati, ufinyu wa bajeti na ulegevu wa uchangiaji wa ada na michango mingine toka kwa wazazi”, alisema Mwalimu Chanafi. 

Naye Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana alimshukuru Mama Kikwete kwa kupata nafasi ya kuitembelea shule hiyo na kumpongeza kwa kazi anayoifanya ya kuinua kiwango cha elimu nchini  na kuendeleza fani yake ya ualimu kwa faida ya kizazi cha leo na kijacho kwa kuwasomesha watoto zaidi ya 600 hawa ni mbali na wanafunzi walioko Shule ya Sekondari WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Mama Kikwete aliichangia shule hiyo mifuko 100 ya simenti  ambayo itatumika kuzima mashimo katika vyumba vya madarasa ambapo wilaya ya Kinondoni itagharamia mchanga pamoja na kumlipa fundi atakayefanya kazi  hiyo.
Mwisho.
Na Anna Nkinda – Maelezo


No comments:

Post a Comment