Balozi Seif akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Kiboje Mamboleo mara baada kuufungua msikiti wao wa Ijumaa uliofanyiwa matengenezo makubwa.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Hassanali akielezea mikakati ya kamati ya ujenzi wa misikiti, Madrasa na maskuli nchini ilivyopania kuendeleza malengo yake.
*********************************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amezikumbusha Kamati za Misikiti hapa nchini kuendelea kuwa imara kwa kutowaruhusu watu wanaopenda kujipenyeza ndani ya kamati hizo kwa nia ya kuanza kutoa madarasa ya uchochezi na kuwagawa waumini kimadhehebu.
Alisema uimara huo ndio njia sahihi itakayoilinda misikiti hiyo na wimbi la vurugu na migogoro ambayo hatiae husababisha mmong’onyoko mkubwa wa ukosefu wa maadili katika jamii za kiislamu.
Akiufungua msikiti mpya wa Ijumaa uliofanyiwa matengenezo makubwa katika Kijiji cha Kiboje Mambo leo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema msikiti ni taasisi yenye mchango mkubwa wa kuutangaza ukweli dhidi ya unafiki pamoja na mambo ya kheri kwa jamii ya Kiislamu.
Balozi Seif alisema katika kuihuisha nyumba ya Mwenyezi Muungu Msikiti ni vyema kwa waumini hao mbali ya kutekeleza vipindi vya sala lakini pia ni vyema wakaendeleza madarasa hasa kipindi hichi kinachokaribia cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kujifunza masuala ya dini yao.
Alisema waumini wa dini ya Kiislamu wanaotekeleza ibada zao na kusimamisha sala katika vipindi vitano kwa siku hupata baraka na neema ya kuwa wageni wa mola wao aliyewaumba.
“ Nani miongoni mwetu hataki kuwa mgeni wa mola wake mara tano ? Kama jawabu ni ndio basi tuhakikishe tunaswali mara tano kama tulivyoamrishwa na mola wetu. Na zile Baraza la manzese zisiwepo tena hapa mtaani penu“. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi wananchi wa maeneo hayo hasa vijana kuachana na maasi ya unywaji pombe kiholela ambayo huchangia vitendo vya wizi wa mazao na mifugo katika maeneo mbali mbali nchini.
Alisema hivi sasa jamii imekuwa ikishuhudia mmong’onyoko mkubwa wa utamaduni wa Kiislamu na kupelekea kuibuka kwa vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa watoto na wanawake kijinsia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi watu wenye kupenda kunywa pombe kuachana na tabia hiyo inayozototesha hata afya zao na badala yake waelekeze juhudi zao katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula kwa lengo la kujijengea hatma njema ya baadaye.
Aliipongeza Kamati ya uendelezaji wa ujenzi wa misikiti, madrasa na maskuli Nchini kwa uamuzi wake wa kuufanyia matengenezo makubwa msikiti huo wa Kiboje Mamboleo ambao ulikuwa katika hali mbaya.
Balozi Seif alielezea imani yake kwamba waumini wa msikiti huo wataendelea kuutunza na kujiepusha na migogoro ya kugombania uongozi ambao hatiae huzaa chuki na hasama zisizo kwisha kwa kipindi kirefu.
“ Misikiti sio sehemu ya kutangazwa sera za siasa kama Viongozi na wahutubu katika baadhi ya misikiti kupendelea kukashifu viongozi waliopo madarakani wakati kinachowapeleka kwenye nyumba hiyo tukufu ni kufanya ibada pekee “. Alifafanua Balozi Seif.
Aliwataka na kuwahimiza waumini hao pamoja na wananchi wa maeneo hayo kuwakataa na kuwatenga watu wote waliojikubalisha kubeba cheche ya shari na utenganifu ndani ya jamii.
Akisoma risala ya waumini na wananchi hao wa Kiboje Mamboleo Ustadhi Juma Abdulla alisema wana jamii hao wameelezea faraja yao kutokana na kumalizika kwa ujenzi wa msikiti huo.
Ustadhi Juma Abdulla hata hivyo alisema bado zipo baadhi ya changa moto zinazoendelea kuwakabili wana jamii hao wa Kiboje Mambo leo ambazo zimekuwa zikiwapa wakati mgumu kwao na kizazi chao.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo Ustadhi Juma alisema kuwa ni pamoja na madrasa, eneo la michezo ya watoto wa kiislamu hasa wakati wa siku kuu pamoja na matengenezo ya chuo cha Qurani kilichopo jirani na msikiti huo.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya usimamizi wa ujenzi wa Misikiti, madrasa na majengo ya skuli hapa Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Hassanali alisema kamati hiyo iliyo chini ya mwenyekiti wake Rais Mstaafu wa Tanzania Alhajj Ali Hassan Mwinyi itaendelea kuongeza nguvu zake kwenye ujenzi wa majengo ya taasisi hizo yenye upungufu hapa Nchini.
Mh. Raza aliwahakikishia wana jamii hao wa Kiboje Mamboleo kwamba uongozi wa Jimbo hilo uko katika jitihada za makusudi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wana jamii hao ikiwemo ya ubovu wa bara bara.
Msikiti wa Kijiji cha Kiboje Mamboleo uliofanyiwa matengenezo makubwa hivi sasa una uwezo wa kusaliwa sala ya kawaida au ile ya Ijumaa na waumini wasiopunguwa mia tatu.
No comments:
Post a Comment