Miamba ya soka barani Afrika Ivory Coast imeimarisha matumaini ya bara hili baada ya kutoka nyuma na kuishinda Japan kwa mabao mawili kwa moja.
Ivory Coast ilijipatia mabao yake kupitia wachezaji Wilfried Bony na aliyekuwa mchezaji wa Arsenal Gervinho huku Japan ikifunga kupitia mshambuliaji wake keisuke Honda.
Ikiwa ni mara ya tatu kwa Ivory Coast kushiriki katika michuano ya Kombe la dunia,haijawahi kufuzu kupitia michuano ya kimakundi.Ushindi huo wa Ivory Coast ni wa kwanza miongoni mwa timu za bara hili na unaiweka timu hiyo sawa kwa pointi na Colombia ambayo iliifunga Ugiriki mabao matatu bila jibu.
Hatahivyo chombo kilikuwa chaenda mrama baada ya kocha Sabri Lamouchi kuwashangaza wengi alipomuacha nje aliyekuwa mshambuliaji wa Chelsea Didier Drogba na kusababisha miamba hiyo kuwa chini kwa bao moja ilipofikia kipindi cha mapumziko.
Japan ambayo ndio mabingwa wa bara Asia walikuwa hatari katika ngome ya Ivory Coast kila walipopata mpira na walifanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya 16 kutoka mshambuliaji wao Honda.
Mchezaji huyo wa kiungo cha kati anayeichezea kilabu ya A.C Milan alipata pasi murwa karibu na lango la upinzani kabla ya kupiga mkwaju mkali uliomuacha mlinda lango wa Ivory Coast kinywa wazi.
No comments:
Post a Comment