Sunday, March 30, 2014

BENK YA NMB YATOA MSAADA WA MADAWATI 100

 Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Kitope waliohudhuria halfa ya kupatiwa Madawati kwa shule za Donge na Kitoe iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Kitope.

  Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akipokea Madawati 50 kwa ajili ya shule ya Sekondari ya Kitope kutoka kwa Meneja wa Tawi la Benki ya NMB Bwana Bakari Khamis Mohd.

   Meneja wa Tawi la Benki ya NMB Bwana Bakari Khamis Mohd akimkabidhi madeski 50 Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Donge.


Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya NMB mara baada ya hafla ya makabidhiano ya madeski kwa ajili ya shule za Donge na Kitope.



Benki ya kuhudumia Wananchi wa Kawaida  Nchini { NMB } imekabidhi mchango wa Madawati 100 kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu katika shule za Sekondari za Donge na Kitope zilizomo ndani ya Wilaya ya Kasakazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Msaada huo wa madawati wenye Thamani  ya shilingi za Kitanzania Milioni Kumi utasaidia kupunguza uhaba wa madeski kwa Shule hizo za Donge na Kitope ambapo kila shule imefanikiwa kupata madeski 50.
Meneja wa Tawi la NBC Zanzibar Bwana Bakari Khamis Moh’d alikabidhi  msaada huo kwa  Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis hafla iliyofanyika hapo katika shule ya Sekondari Kitope.
Meneja huyo wa Tawi la Benki ya NMB Bwana Bakari aliiomba Jamii kuendelea kuiunga mkono Benki hiyo ili kusaidia kuipa nguvu za kiutendaji itakaoongeza kasi ya kusaidia harakati za Kijamii Nchini.
Alisema Benki hiyo tokea kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1997 imekuwa ikijitahidi kuunga mkono maendeleo ya Wananchi hasa katika miradi iliyomo ndani ya Sekta ya Elimu.
Akitoa shukrani zake mara baada ya kupokea msaada huo wa madawati Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziomba Benki nyingine Nchini kuiga mfano wa Benki ya NMB katika kusaidia maendeleo ya Wananchi.
Balozi Seif alisema taasisi za Kifedha ndani na nje ya nchi zimekuwa na mfumo maalum unaosaidia kuunga mkono juhudi za jamii katika maeneo tofauti ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Alisema Wananchi hawanabudi kushirikiana na kuzipa nguvu taasisi hiyo ili ziweze kutekeleza malengo zilizojipangia.

“ Ukweli halisi NMB ni Benki ya wanyonge. Ni Benki yetu inayolenga kuhudumia wananachi wa kipato cha chini. Huyu ndie rafiki yetu na tunapaswa kumuunga mkono “. Alisema Balozi Seif.
Naye Mbunge wa Jimbo la Donge  Mh. Sadifa Juma Khamis alisema Benki ya NMB imeonyesha umahiri mkubwa katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010  ambayo imejipangia kuimarisha Sekta ya Elimu iliyo  muhimili pekee wa maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa lolote Duniani.
Akisoma risala ya Walimu na wazazi wa Skuli za Donge na Kitope Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Suleiman  Juma Makame ameupongeza Uongozi wa Benki hiyo pamoja na ule wa Jimbo la Kitope kwa juhudi zao zilizojikita zaidi katika kuimarisha Sekta ya Elimu.
Hata Hivyo Mwalimu Suleiman alisema zipo changa moto zinazoendelea kuzikabili shule hiyo akatolea mfano wa shule yake ya Kitope inayokabiliwa na uhaba wa Vifaa vya Maabara pamoja na uwezekwaji wa jengo moja la Shule hiyo.
Akitoa  salamu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Afisa  Elimu wa Wilaya ya Kaskazini “B “ Mwalimu Ussi Machano alieleza kwamba mchango wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif katika Sekta ya Elimu umekuwa mfano wa kuigwa na Viongozi wengine hapa Nchini.
Mwalimu  Ussi Machano alisema kwamba mchango huo kwa kiasi kikubwa umeipunguzia mzigo mkubwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika     ukamilishaji wa Majengo mbali mbali ya Shule yanayoanzishwa na wananchi wenyewe kwa mpango wa kujitolea.
Huu ni mkupuo wa Pili kwa Benki hiyo ya NMB kusaidia madawati kwa Shule za Donge na Kitope.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment