Jangwani au Chamazi? Shomary Kapombe anataka kucheza timu ambayo itashiriki michuano ya Afrika mwakani. *********************************************************** Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam SHOMARY Kapombe ameamua kurejea nyumbani Tanzania kutoka Ufaransa, lakini anataka kucheza klabu ambayo itashiriki michuano ya Afrika mwakani- maana yake, uwezekano wa kurejea Simba SC sasa unakuwa mdogo. |
Kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia, anamaliza Mkataba wake Simba SC mwezi ujao, lakini alikwishaingia Mkataba wa miaka minne na AS Cannes ya Ufaransa mwaka jana.
Na Simba SC imekubaliana na klabu ya Daraja la Nne Ufaransa, kuununua Mkataba wa mchezaji huyo arejee kufanya kazi Msimbazi baada ya kushindwa kuendelea kucheza Ulaya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alizungumza na AS Cannes mwezi uliopita na kufikia makubaliano ya kuuziana Mkataba huo, ili Kapombe arejee Msikmbazi.
Poppe alisema kwamba Simba SC imekubali kuilipa Cannes kiasi cha Euro 33, 000 ambazo sawa na Sh. Milioni 66 ili kurejeshewa mchezaji wake huyo.
Kapombe alitolewa bure kwenda AS Cannes katikati ya mwaka jana akiwa bado ana Mkataba na klabu hiyo ya Msimbazi, unaomalizika Aprili mwaka huu.
Baada ya kuwa Ufaransa kwa zaidi ya miezi mitatu, Kapombe alirejea nchini Novemba mwaka jana kwa ruhusa maalum ya kuja kuichezea timu ya taifa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe.
Baada ya mchezo huo, mchezaji huyo akaamua kubaki moja kwa moja nyumbani akidai halipwi mishahara.
Kapombe mwenyewe amekuwa mgumu kuzungumzia suala hilo, lakini tayari kuna habari kwamba Yanga SC na Azam zinamtaka pia mchezaji huyo.
Yanga SC na Azam FC ndizo zipo kwenye nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, hadi sasa zikiwa zinakimbizana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Azam FC ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 50 ilizovuna katika mechi 22, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46, lakini wana mchezo mmoja mkononi.
Wakati Yanga SC imebakiza mechi tano na Azam FC nne, mchuano wa kuwania ubingwa unaonekana kuwa mkali zaidi baina ya timu hizo mbili na mechi za Jumapili zinatarajiwa kutoa picha zaidi ya mbio zao.
Azam FC ikiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Simba SC, wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Yanga SC watahamia Mkwakwani, Tanga kuwakabili Mgambo JKT
No comments:
Post a Comment