Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tumepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata sh. milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.
Tayari tumeanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa Machi 22 mwaka huu mjini Tabora tumezuia sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa mgawo wa Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya sh. 38,655,000.
Wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106.
Tunawakumbusha wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu, vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na vyama shiriki) kuzingatia mikataba wanayoingia na watendaji wao wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine.
Iwapo wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate taratibu kwa vile hakuna mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande mmoja unataka kufanya hivyo.
*AZAM, YANGA VIWANJANI DAR, TANGA VPL
Timu za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara zinashuka tena viwanjani kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania pointi tatu.
Azam yenye pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mgambo Shooting ipo katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL ikiwa na pointi 19.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga ipo nyuma ya Azam kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47. Hata hivyo, timu hiyo ina mchezo mmoja mkononi.
Tanzania Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David Mwamaja hivi sasa ina pointi 22 ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za mwisho katika ligi hiyo itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Ligi itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ashanti United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Jumapili (Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu), JKT Ruvu na Rhino Rangers (Uwanja wa Azam Complex), Azam na Simba (Uwanja wa Taifa) na Mgambo Shooting na Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).
*KAMATI YA SHERIA KUPITIA MAREKEBISHO YA KATIBA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana mwishoni mwa wiki kupitia taarifa ya utekelezaji wa agizo la wanachama kurekebisha katiba zao.
TFF tulitoa agizo kwa wanachama wetu kufanyia marekebisho katiba ikiwemo kuingiza Kamati ya Maadili. Mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo ulikuwa Machi 20 mwaka huu.
Hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itapokea taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa Sekretarieti, na baadaye kutoa mwongozo wa hatua inayofuata.
*TIMU YA WATOTO WA MITAANI YAENDA BRAZIL
Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza imeondoka leo (Machi 26 mwaka huu) kwenda Brazil kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani.
John Kadutu ambaye ni mjumbe wa Bodi ya kituo hicho, na pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha klabu za Mkoa wa Mwanza ndiye kiongozi wa msafara wa timu hiyo ya Tanzania.
Michuano hiyo ya siku 10 inayoshirikisha watoto wa mitaa (wavulana na wasichana) inaanza keshokutwa (Machi 28 mwaka huu). Nchi 19 zinashiriki michuano hiyo itakayofanyika katika Jiji la Rio de Janeiro.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kwa upande wa wavulana ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na Zimbabwe.
Mwaka 2010 mashindano hayo yalifanyika Durban, Afrika Kusini ambapo pia Tanzania ilishiriki.
*MABINGWA WA MIKOA WATAKIWA MACHI 30
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linavikumbusha vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwa vinatakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao kufikia Machi 30 mwaka huu.
Majina ya mabingwa yanatakiwa kuwasilishwa pamoja na usajili wa wachezaji waliotumika kwenye ligi ya mkoa. Kila klabu inaruhusiwa kuongeza wachezaji watano kutoka ndani ya mkoa husika, ambapo unatakiwa uthibitisho wa usajili huo.
Mpaka sasa ni vyama viwili tu ndivyo vimeshawasilisha mabingwa wao. Vyama hivyo ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ambapo bingwa wake ni Kiluvya United, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi (LIREFA) ambapo bingwa ni Kariakoo SC
No comments:
Post a Comment