Monday, March 31, 2014

*WIZARA YA AFYA YAELEZEA MPANGO WA UPIMAJI AFYA WANANCHI KWA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

 Meneja Masoko  na Elimu kwa Umma  toka  Mfuko  wa Taifa wa Bima ya Afya  (NHIF) Bi Anjela Mziray akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam kuhusu programu ya upimaji wa Afya kwa wananchi kwa magonjwa yasiyoambukiza inayoendeshwa na mfuko huo hapa nchini. Kulia ni Meneja Uhakiki na Madai wa mfuko huo Dk.Clement Masanja na kushoto ni Afisa habari ,Idara ya Habari Maelezo  Bi Fatma Salum.
 Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uliofanyika leo jijini Dar es salaam uliolenga kuelimisha wananchi kuhusu mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama Kisukari,shinikizo la damu na Saratani.
************************************
Na frank Mvungi-Maelezo
Serikali yaweka mikakati madhubuti kupambana na magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini.

Hayo yamesema na  Meneja Masoko  na Elimu kwa Umma  toka  Mfuko  wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF) Bi Anjela Mziray  wakati wa mkuatano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

Akieleza Bi Anjela amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa  Bima ya Afya imekuwa ikichukua juhudi za maksudi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu na Saratani za aina mbalimbali.

Akifafanua zaidi Bi Anjela amesema programu hiyo imekuja kutokana na ukweli kwamba magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka na yamekuwa tishio na kusababisha vifo vya watu wengi nchini na duniani ambapo takwimu za shirika la afya Duniani za mwaka 2012/2013 watu zaidi ya milioni 35 hufa kwa sababu ya magonjwa yasiyoambukiza.

Bi Anjela aliongeza kuwa kati ya waathirika wa magonjwa yasiyoambukiza milioni 28.1 wanatoka katika nchi zinazoendelea ambapo kwa Tanzania magonjwa hayo husababisha vifo mara 4 zaidi mijini ambavyo ni sawa na  asilimia 12.8 wakati asilimia 3.1 wapo vijijini.

 Akitolea Mfano Bi Anjela alisema katika zoezi la upimaji lililofanyika Dodoma Septemba, 2013 jumla ya watu 591 walipimwa kati yao 14  sawa na asilimia 2.3 waligundulika kuwa na kisukari, na 28 sawa na asilimia 5 walikuwa na shinikizo la damu, wakati  watu 128 sawa na asilimia 22 walikuwa na uzito uliokithiri.
Bi Anjela aliongeza kuwa katika zoezi lililofanyika Mlimani City Jijini Dar es salaam ocktoba, 2013 watu 450 walipimwa, nusu yao waligundulika kuwa na uzito uliokithiri na katika zoezi lililofanyika Zanzibar watu 273 walipimwa ambapo kati yao watu 10 sawa na asilimia 3.6  waligundulika kuwa na kisukari, watu 83 sawa na  asilimia 30.4 walikuwa na uzito uliokithiri.

Naye  Meneja Uhakiki na Madai wa mfuko huo Dk.Clement Masanja  alitoa wito kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi  na kuzingatia lishe bora ili kujikinga na magojwa yasiyoambukiza kama kisukari, msongo wa mawazo  na shinikizo la damu.


Katika jitihada za Kutoa huduma bora kwa wananchi  Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umebuni mkakati maalum ambao unajulikana kama Afya Bonanza ambayo ni Kampeni ya kupima afya na kutoa elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza  na inakusudiwa kufanyika mikoa yote hapa nchini ambapo  Zoezi hilo lilizunduliwa rasmi Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam  mwezi machi 2014

No comments:

Post a Comment