TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana iliwatoa kimasomaso Watanzania baada ya kuilaza Zimbabwe bao 1-0 katika mchezo wa awali wa michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika uliofanyika katika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, Taifa Stars sasa inahitaji sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo mjini Harare.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi kwa kila timu kushambulia lango la mwenzake ambapo katika dakika ya tatu, Stars walikosa bao wakati John Bocco alipounganisha kwa kichwa krosi ya Thomas Ulimwengu, lakini mpira ulidakwa na kipa George Chigova wa Zimbabwe.
Zimbabwe nayo ilijibu mashambulizi ambapo katika dakika ya 11, shuti lililopigwa na Mahachi lilidakwa na kipa Munishi wa Stars.
Stars iliendeleza mashambulizi katika lango la Zimbabwe na katika dakika ya 13, Bocco aliandika bao pekee na la ushindi baada ya kumalizia vyema pasi iliyopigwa na Ulimwengu.
Baada ya bao hilo, kila timu iliongeza kasi ya mashambulizi huku Zimbabwe ikihaha kusawazisha bao hilo.
Mashambulizi hayo yaliendelea kwa kila upande kushambulia lango la mwenzake na hadi mapumziko, Stars ilikuwa ikiongoza kwa bao hilo moja dhidi ya Zimbabwe.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikishambulia ngome ya mwenzake. Hata hivyo, Zimbabwe ilitawala mchezo huku ikitafuta bao kwa nguvu zote, lakini hadi kipenga cha mwisho, Stars ilimudu kulilinda goli lake.
Stars: Deogratius Munishi,Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.
Zimbabwe: George Chigova, Partson Jaure ,Danny Phiri, Hardlife Zvirekwi, Stephen Alimwenda, Tendai Ndoro, Milton Nkube,Kudakwashe Manachi, Curthbert Malajila Peter Moyo na Eric Chipeta.
No comments:
Post a Comment