Sunday, May 18, 2014

TIMU YA JKT RUVU KUANZA MCHAKATO WA KUTAFUTA VIPAJI

Timu ya JKT Ruvu leo itaanza mchakato wa kutafuta wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye uwanja wa JKT Mlalakuwa jijini.

Zoezi la kusaka wachezaji hao ni la wazi na meneja wa timu hiyo, Joel Frank amewataka wachezaji wote wenye nia ya kucheza ligi kuu msimu ujao kufika kwa wingi katika uwanja huo kuanzia saa 1.30 asubuhi.
Frank alisema kuwa wameamua kutafuta wachezaji kwa mtindo huo kwa lengo la kuona uwezo wao halisi na wala si kwa kukisia kama ilivyokuwa kwa timu nyingine.
Alisema kuwa zoezi hilo litasimamiwa na kocha wao mkuu, Fred Felix Minziro kwa kushirikiana na wasaidizi wake, Azishi Kondo na Greyson Haule.
“Hatusajili kwa kufuata majina, sisi ni tofauti na timu nyingine, tumeamua kubadili mfumo wa kusajili kwa mazoea na sasa tunasajili kwa kuona uwezo wa mchezaji mwenyewe uwanjani si kwa kusikia,” alisema Frank.
Alisema kuwa zoezi hilo litaendeshwa kwa wiki moja na pia linahusisha wachezaji wanaotaka kucheza timu yao ya chini ya miaka 20 (U 20).
“Hii ni fursa kwa wachezaji wenye uwezo na tunahitaji wachezaji 10 kwa ajili ya msimu ujao. Kamwe hatutasajili kwa kufuata wachezaji katika timu nyingine, sis tunasajili uwanjani na tunawaomba wajitokeze kwa wingi,” alisema.
Aliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuepuka matatizo waliyokumbana nayo katika msimu uliopita na pia kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza.
“Tumechoka kushiriki, tunataka kutwaa ubingwa msimu ujao, msimu uliopita tulianza vizuri, tukapatwa na matatizo na kupoteza nafasi, tumeweka mikakati mipya na kwa sasa tumeanza kuifanyia kazi, tunauhakika itafanikiwa,” alisema.
Na Mwandishi wetu

No comments:

Post a Comment