Wednesday, February 26, 2014

*HABARI KUTOKA TFF LEO

*SYMBION KUSAIDIA PROGRAMU ZA VIJANA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Symbion Power Tanzania Limited zimesaini makubaliano ambapo kampuni hiyo itasaidia kwenye maeneo matatu ya mpira wa miguu wa vijana.

Makubaliano hayo yametiwa saini leo (Februari 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam. Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati upande wa Symbion aliyesaini ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Peter Gathercoles.

Maeneo ambayo Symbion itasaidia ni ujenzi wa vituo viwili vya kuendeleza vipaji vitakavyojengwa Kidongo Chekundu na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mashindano ya Taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 12 (U12) yatakayofanyika mwaka huu na kuisaidia timu ya U17 ya Tanzania (Serengeti Boys).

Serengeti Boys itacheza na Afrika Kusini, Julai mwaka huu katika mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa wachezaji wa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger.

Hivyo Symbion imetoa dola 60,000 (zaidi ya sh. milioni 96) kwa ajili ya mashindano ya U12, na dola 50,000 (zaidi ya sh. milioni 80) kwa ajili ya maandalizi ya Serengeti Boys kwa mechi dhidi ya Afrika Kusini.

Rais Malinzi ameishukuru Symbion kwa kukubali kushirikiana na TFF katika mpira wa miguu wa vijana, lakini vilevile amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwani ndiye chachu ya kampuni hiyo kuamua kujishirikisha na mpira wa miguu wa vijana.

*ZAMBIA WATUA KUIKABILI TWIGA STARS
Timu ya Taifa ya Zambia (Shepolopolo) inatua nchini kesho mchana (Februari 27 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Tanzania (Twiga Stars) itakayochezwa keshokutwa (Februari 28 mwaka huu).

Shepolopolo yenye msafara wa watu 29 itawasili kwa ndege ya Fastjet ikitokea Lusaka na itafikia kwenye hoteli ya Accomondia kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni.

Waamuzi wa mechi hiyo kutoka Burundi wakiongozwa na Ines Niyosaba wamewasili nchini leo asubuhi wakati Kamishna Fran Hilton-Smith kutoka Afrika Kusini atawasili kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya South African Airways.

*RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari juu ya benchi la ufundi la timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars).


Mkutano huo utafanyika kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.

*CHAMA cha Mapinduzi (CCM), chajiingiza matatani baada ya kuwapangisha wafanyabiashara wawili katika flemu moja

indexCHAMA cha Mapinduzi (ccm), kimejiingiza matatani baada ya kuwapangisha wafanyabiashara wawili katika flemu moja ya kufanyia biashara.  Akizungumza jana jijini Dar es Salaam mfanyabishara Charles Msigwa alisema aliingia mkataba na Mecy Mziray ambaye kwa sasa ni marehemu na aliendelea kumlipa kodi ndugu wa marehemu Vesta Haule. 

Alisema wakati akiendelea kufanya biashara katika banda hilo alishangazwa na viongozi wa CCM tawi la Vigaeni Kata ya Ndugumbi kumfuata wakitaka aingie mkataba upya na chama hicho. 

“Nimekuwa nikiendesha shughuli zangu za biashara kwa muda wa miaka minne ndipo nilipofuatwa na viongozi wa CCM na kunishauri nichukue mkataba nao ili chama kipate mapato,”alisema Msigwa. 

Aliongeza kuwa viongozi hao walimuita kwenye ofisi ya tawi na kumuhakikishia hakutakuwa na tatizo lolote juu ya mkataba huo. “Viongozi hao waliniambia kuwa mabanda hayo hayarithishwi hata hivyo aliyeachiwa amekuwa msumbufu wa kodi mwenye banda alishafariki kwa hiyo banda huwa linarudi na kuwa mali ya chama,”alisema. 

Msigwa alisema kuwa aliujaza mkataba huo na kuurudisha ofisini kwao alipotaka kuulipia akawa anazungushwa zungushwa. 

“Nilipeleka malalamiko yangu Kwa uongozi wa Wilaya ambapo uliwaandikia barua ya kwamaba wanitafutie banda jingine iwapo nikiwa tayari kutimiza masharti ya kuwa mpangaji wa chama hicho na nilikubali lakini uongozi huo haukufanya kama ulivyo agizwa,”alisema Msigwa. 

Awali Chama cha mapinduzi (CCM) kiliingia mkataba wa kujenga banda hilo na Marehemu Mecy Mziray gharama zake na asingeweza kutoka mpaka gharama zake za ujezi zitakapo malizika.