Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Ujumbe wa Chama cha Ukombozi cha nchini Palestina (PLO) uliofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam jana Juni 14, 2013 kwa ajili ya mazungumzo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Chama cha Ukombozi cha Palestina (PLO), Tayseer Khalid, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini Kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam.
**********************************************
Na Mwandishi Maalum, Dar es salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na ujumbe wa Chama cha Ukombozi cha Palestina (PLO) ambapo wamezungumzia umuhimu wa kuimarisha uhusiano uliopo wa muda mrefu baina ya Tanzania na Palestina.
Ujumbe huo wa watu watano ambao unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya PLO Tayseer Khalid upo nchini kwa ziara yenye lengo la kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mazungumzo hayo, yaliyofanyika jana ofisini kwake Ikulu, Dkt. Bilal alisema uhusiano huo uliodumu kwa muda mrefu unapaswa kuthaminiwa na kuimarishwa na serikali zote mbili.
Dkt. Bilal alitumia fursa hiyo kuipongeza Palestina kwa kukubalika kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) pamoja na kupata nafasi ya kuwa mshiriki katika Umoja wa Mataifa na kusema huo ndiyo mwanzo wa mafanikio kwa Taifa hilo.
Naye Tayseer Khalid alielezea furaha yao kwa ujumbe huo kuja Tanzania nchi ambayo hawataisahau kwa misimamo yake ya kutetea haki tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa kiongozi wa Palestina Yasser Arafat. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Katibu wa NEC-CCM Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dkt. Asha-Rose Migiro.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Comoro kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, ujumbe uliokabidhiwa kwake na Waziri wa Ulinzi wa Comoro Hamada Madi.
No comments:
Post a Comment