Friday, June 21, 2013

*WATANZANIA WATAKIWA KUKESHA WAKIOMBA AMANI KWA IMANI ZAO


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abas Kandoro,


Na Anna Nkinda – Maelezo, Mbeya
Watanzania wametakiwa kupiga magoti na kuomba kila mtu kwa imani yake ili mwenyezi Mungu aweze kuwalaani watu ambao wanatishia kuvuruga amani ya nchi na kusababisha chuki katika jamii.

Wito huo umetolewa leo na Chifu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Rocket Mwashinga wakati akiongea na wakazi wa Ushirika wilayani Rungwe kwenye  mazishi ya George Mwaikela aliyefariki Dunia juzi jijini Dar es Salaam kwa ajali ya gari.

Chifu Mwashinga alisema kuwa hali iliyopo nchini hivi sasa si nzuri kwani kuna baadhi ya makundi ya watu wanataka kuwalambisha watanzania sumu mbaya ya chuki ya udini na kuwaomba wasiilambe sumu hiyo bali kila mmoja kwa imani yake apige magoti na kumuomba Mwenyezi Mungu ili amani iliyopo iendelee kuwepo.

“Tunashindwa kulala  usingizi kutokana na hofu na katika mkusanyiko kama huu tunakosa raha kabisa kwa kuhofia kuwa jambo baya lolote linaweza kutokea”, alisema Chifu Mwashinga.

Alisema kuwa marehemu George alikuwa ni kijana mdogo wa kwanza na wa ajabu  aliyeweza  kuwafuata mashifu na kuwapa ushauri mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuata mila nzuri na kuachana na mila ambazo zimepitwa na wakati. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abas Kandoro  alisema kuwa binadamu anaweza kupata madhara  kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu na katika kitu kibaya ambacho  kinaanza kutokea katika jamii ya watanzania ni pamoja na kubaguana katika misingi ya dini hali ambayo itasababisha watu kuuana.

Mh. Kandoro alisema, “Tumekusanyika hapa kuja kumzika ndugu yetu si kwa itikadi ya dini bali ni binadamu mwenzetu, tulikuwa tunaishi naye kwa amani na upendo na sisi sote mbele ya Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja na matendo yetu katika dunia ndiyo yatakayotufanya  tuuone ufalme wa Mungu.
Sisi kama viongozi wenu wa Mkoa huu tunawaomba mdumishe amani na utulivu tulionao ili tuweze  kufanya mambo makubwa kama wanayofanya watu wengine”.

Naye  Baba Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Ruanda Padre Peter Malya  aliwataka watanzania kuishi  maisha yanayoendana na ubinadamu  na ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na kuachana na matendo ya kinyama.

Padre Malya alisema kuwa hivi sasa kuna baadhi ya watu wanauza mkaa, juu ya magunia wanapanga mkaa mkubwa na mzuri lakini chini wanaweka chenga na wengine wanauza nyanya, juu ya ndoo wanaweka  kubwa na nzuri lakini chini wanaweka ndogo na wengine wamefikia hatua ya kuhifadhi  samaki kwa kutumia dawa za kuhifadhia maiti.

“Ninawaomba muishi kwa upendo na kuwasaidia watu wasiojiweza wakiwemo   yatima, wajane, wagonjwa  na vikogwe na kwa kufanya hivyo mtakuwa mnajiongezea baraka kwa Mwenyezi Mungu na kuacha kumbukumbu pale ambapo mtakuwa mmeaga Dunia na kutangulia mbele za haki”, alisema Padre Malya.


Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali walihudhulia mazishi hayo akiwemo Mke wa Rais Mh. Mama Salma Kikwete na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mh. Adam Malima

No comments:

Post a Comment