Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Mbeya
Taasisi ya Wanawake na Maendelea (WAMA) imetoa msaada wa cherehani ya kudarizi kwa mjane Fatma Almasi ambaye ni mkazi wa Ilomba jijini Mbeya.
Makabidhiano ya Cherehani hiyo yalifanyika hivi karibuni Ikulu jijini Mbeya.
Akimkabidhi cherehani hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa moja ya kazi anazozifanya ni kumuinua mwanamke kiuchumi hivyo basi alitoa cherehani hiyo ili iweze kumsaidia mjane huyo katika maisha yake.
Mama Kikwete alisema kuwa cherehani hiyo ni moja ya vyerehani walivyovipata kutoka nchini China kwani watu wanapoomba kusaidiwa siyo kama vitu wanavyovihitaji vipo bali nao wanatafuta sehemu mbalimbali wakipata wanafikisha kwa wahitaji.
“Nakutakia kila la heri katika kazi zako ila usisahau kuleta mrejesho kama kazi inaendelea au la, isije ikatokea baada ya muda cherehani ikauzwa hiyo siyo maana yake bali ifanye kazi ya kuzalisha ili nawe uweze kujiinua kiuchumi”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Fatma Almasi alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada aliompatia kwani amekuwa akihitaji kuwa na cherehani ya kudarizi kwa kuwa uwezo wa kudarizi anao lakini hakuwa na kitendea kazi na aliahidi kuongeza cherehani kingine kutokana na nguvu zake mwenyewe.
Fatma alisema, “Kinamama tujitahidi kujikwamua kimaisha kwani mwanamke akiwezeshwa anaweza, tusiwe wategemezi kwa kina baba na mtu asijione kuwa yeye ni mjane au anaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hawezi kufanya jambo lolote na kuona kuwa ni mwisho wa maisha bali ajitahidi kuwa mjasiriamali kwa kufanya hivyo ataweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha”.
Aliwaomba wanawake kumuunga mkono na kumtia nguvu Mama Kikwete kwani ana moyo wa huruma na upendo wa kuwasaidia kina mama na watoto wa kike.
Taasisi ya WAMA imekuwa ikiwainua wanawake kiuchumi, kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha afya ya mama wajawazito na watoto na kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
No comments:
Post a Comment