Monday, June 24, 2013

*SHEHA ALIYEMWAGIWA TINDIKALI ZANZNIBAR AANZA MATIBABU NCHINI INDIA

Sheha wa Shehia ya Tomondo Mohd Omar Said { Kidevu } wakati alipokuwa akipatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kwa takriban mwezi mmoja kabla ya kupelekwa Nchini India ambako ameanza uchunguzi na  matibabu zaidi. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
*****************************
Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Miot Mjini Chenai Nchini India leo wanaanza kumfanyia huduma za matibabu Sheha wa shehia ya Tomondo  Mohd Omar Said { Kidevu } baada ya kukamilisha uchunguzi wa matatizo yake kufuatia kumwagiwa Tindi kali karibu mwezi mmoja uliopita.
Sheha Kidevu aliyefika Nchini humo Tarahe 21 na kufanyiwa vipimo vyote vilivyohusika anaanza matibabu kwa hatua ya kupandikizwa ngozi katika sehemu zake alizoathirika kutokana na kuungua kwa maji ya Tindi kali hiyo.
Akizungumza kwa njia ya Simu Daktari aliyeambatana  na Sheha huyo Dr. Said Ali Said { Mkarafuu } alieleza kwamba Madaktari wa India wameelezea kuridhishwa kwao na hatua kubwa iliyochukuliwa na Madaktari wa Zanzibar ya kumpatia tiba sahihi mgonjwa huyo.
Dr. Said alisema Madaktari hao Bingwa wa India wamekaririwa wakisema kwamba wamepata matumaini ya huduma hizo alizofanyiwa Zanzibar ambazo zinawapa hatua ya pili ya kuendelea na Tiba ya Sheha Kidevu.
“ Amefanyiwa  uchunguzi wa vipimo vyote na kubainika kwamba jicho lake Sheha Kidevu ambalo liliwahi kupata athari kidogo limewahiwa na Madaktari wa Zanzibar  wakiongozwa na Dr. Gang na Dr. Slim na hivi sasa liko katika hali ya kawaida “. Alifafanua Dr. Said Mkarafuu.
Alifahamisha kwamba Madaktari hao wa Hospitali ya Miot Mjini Chenai Nchini India wameelezea matarajio yao kwa mgonjwa huyo kuendelea na huduma za matibabu kwa haraka licha ya Madaktari hao kutokutaja huduma hizo zitamalizika katika kipindi gani.
Kabla Sheha Mohd Kidevu alikuwa akipatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kwa takriban Mwezi Mmoja sasa kutokana na kuathirika  sehemu ya kulia ya kifua chake, Bega pamoja na baadhi ya maeneo ya mapaja.
Sheha huyo wa Shehia ya Tomondo Mohd Omar Said Kidevu alipatwa na mtihani huo wa kumwagiwa Tindi kali { Acid }  na mtu asiyejuilikana Usiku wa tarehe 22 Mei Mwaka huu wa 2013 akiwa katika harakati za kuteka Maji mara baada ya kurejea kwenye Ibada ya sala ya Ishaa.
Vitendo vya matumizi mabaya ya tindikali vinavyofanywa na baadhi ya watu vinaonekana kuanza kuwatia hofu wananchi na hasa baadhi ya Viongozi katika maeneo mbali mbali hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment