HALI ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema) Joshua Nassari,aliyehamishiwa juzi katika Hospitali ya Taifa ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam, akitokea Hospitali ya Silian jijini Arusha, inaendelea kuimarika.
Mbunge huyo alipigwa na watu aliowaita kuwa ni wanachama wa CCM Juni 16 mwaka huu kwenye vurugu za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni Wilayani Monduli Mkoani Arusha.
Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu, msemaji wa MOI Almas Jumaa, alisema kuwa hali ya Mbunge huyo, kwa sasa inaendelea kuimarika ingawa bado analalamika kuwa anahisi maumivu makali shingoni na mgongoni, lakini bado anaendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
“Hali ya mgonjwa inaendelea kuimarika ingawa bado analalamika maumivu ni makali eneo la shingoni na mgongoni,kuna vipimo ambavyo amefanyiwa na madaktari wake wanaendelea kuvitafiti ili kubaini tatizo zaidi,”alisema Jumaa.
Akizungumzia hali yake, Nassari alisema amepimwa kipimo cha X-ray ambapo kimeonyesha kuwa pingili za mgongo wake zipo sawa, lakini daktari ameshauri afanyiwe kipimo kingine kiitwacho MRI ili kuangalia hali ya mishipa kutokana na maumivu makali anayoendelea kuyapata.
No comments:
Post a Comment