Monday, August 20, 2012

Full Yanga 4-African Lyon 0, Msuva ang'ara


Kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga, Haruna Niyonzima (kulia) akimsakata kiungo wa  African Lyon, wakati wa mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara, inayotarajia kuanza hivi karibuni, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, leo jioni. Katika mchezo huo Yanga imeibuka na ushindi wa Mabao 4-0. Bao la kwanza la Yanga, limefungwa na kipa wa African Lyon, Juma Abdul, aliyejifunga katika dakika 8, kipindi cha kwanza, bao la pili limefungwa na Haruna Niyonzima kwa mkwaju wa penati, dakika ya 54, baada ya beki wa Lyon Semi Kessy, kumchezea rafu, Msuva katika eneo la hatari. Goli la tatu limefungwa na Simon Msuva, katika dakika ya 72, kufuatia pasi safi ya Frank Dumayo na bao la nne limefungwa na Jerry Tegete katika dakika ya 90+2, baada ya pasi safi ya Idrisa Rashid.
 Replay ya Penati iliyosababishwa na Simon Msuva (kushoto) akimsakata Beki wa African Lyon, Semi Kessy.
 Msuva, kapita, beki kazidiwa kaanza jitihada za ziada kumzuia kwa mkono.......
 Bado haitoshi aliona anazidi kuzidiwa, ikabidi atumie mkono na miguu kwa kumtega kwa nyuma.....
 Akaona isiwe tabu Heri lawama kuliko Fedheha.......akamaliza kazi ndani ya eneo la hatari la penati Boksi.....
 Mwamuzi wa mchezo huo akaamuru penati, hapa kipa wa African Lyon, akatoka kabla ya kupigwa mkwaju huo na Niyonzima na kupangua, mwamuzi huyo akaamuru irudiwe penati hiyo......
 Iliporudiwa, kipa huyu aliteswa kama hivi, Mpira kulia kwake yeye kushoto kwake.........Goooooooo!!!!! la tatu.
Goli lililoonekana kuzua utata kama inavyoonekana beki wa Lyon, akiokolea nyuma ya mstari....
Kocha wa timu ya Africa Lyon, Muargentina,  Pablo  Velez, akionekana kulalamikia jambo kwenye benchi la ufundi la timu yake  wakati timu yake ilipokutana na timu ya Yanga katika mchezo wa kirafiki kwenye uwanja wa Taifa jioni hii.
Kikosi cha timu ya Africa Lyon.
Kikosi cha timu ya Yanga. 

Saturday, August 18, 2012

Miss Tanzania aja na Filam ya Kisa cha kifo cha Kanumba

Miss Tanzania No. 3, 2009, Julieth William Lugembe nyota wa filamu mpya ya "Sister Julieth"

Miss Tanzania No. 3, 2009, Julieth William Lugembe (kushoto) na Sylvia Shally Miss TZ No.4 2009 ambao wamecheza filamu mpya ya "Sister Julieth"

MISS Tanzania Na.3 wa mwaka 2009, Julieth William amemshirikisha mrembo mwenzake aliyeshika Na.4 mwaka huo, Sylvia Shally, katika filamu mpya inayokwenda kwa jina la "Sister Julieth".

Filamu hiyo ambayo iko katika hatua ya uhariri inaelezea kisa cha kijana ambaye anatuhumiwa kumuua rafikiye wa kike wakati wakiwa peke yao chumbani na kesi mahakamani inamuelemea kijana huyo.

Sister Julieth, nafasi ambayo inachezwa na Sylvia, anakuja kama mzimu na kumtetea kijana huyo, ambaye anakumbana na upinzani mkali kutoka kwa mawakili wa upande wa mashitaka. 

Mrembo huyo aliyegeukia katika uigizaji, alisema hii ni filamu yake ya kwanza kucheza, kama ilivyo kwa Sylvia na kwamba ameitunga yeye mwenyewe.

Baada ya mwandishi kuhoji kama filamu hiyo inahusiana na tukio la marehemu Steven Kanumba aliyefariki wakiwa peke yao chumbani na muigizaji Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, aling'aka: "Aaah hapana. Hata kidogo. Ni kisa tofauti kabisa. Ni kisa kinachouhusisha mzimu unaokuja duniani kutoa ushahidi. 

"Ni kati ya filamu za hisia kali. Iko katika hatua ya uhariri na wakati wowote itatoka." 

Alisema katika filamu hiyo amewashirikisha pia wasanii wengine maarufu akiwamo Dude.

Katika shindano la Miss Tanzania 2009 ambalo Julieth alishika Na.3, Miriam Gerald aliibuka mshindi wa kwanza, Beatrice Lukindo alikuwa wa pili wakati nafasi ya nne ilishikwa na Sylvia na Sia Ndaskoi alikamilisha Top 5.

Thursday, August 16, 2012

Stars yatoka sare ya 3-3 na Botswana ‘Zebras’ kwao


 Mabeki wa Taifa Stars, wakimwangilia mshambuliaji wa Botswana ‘Zebras’ akifunga bao la tatu, wakati wa mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa Molepolole mjini Gaborone, jana.
Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana, ‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
 Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana, ‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa na Lemponye Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja. Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum Abubakar na nafasi zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman Idd.
Safari hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika 13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa mara ya kwanza.
Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo/Shabani Nditi, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd, Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi Kazimoto.
Zebras; Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.