Tuesday, July 19, 2016

*SIMBA NA YANGA KUKIPIGA OKTOBA 1 MWAKA HUU


 Na Ripota wa Sufianimafoto Blog, Dar 
BAADA ya Simba kutofanya vizuri katika Ligi msimu uliopita kwa kukubali kunyanyaswa na watani wao wa Jadi katika soka la Bongo, Yanga, hatimaye mtanange wa upinzani na kutambiana baada ya usajili wa kila upande baina watani hao, unatarajiwa kupigwa Oktoba Mosi, mwaka huu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar esSalaam, leo Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema kuwa mujibu wa ratiba mpya iliyotolewa na Shirikisho hilo leo mchezo huo utakuwa ni wa raundi ya saba ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Aidha baada ya kusambaa kwa Ratiba hiyo katika mitandao mbalimbali ya kijamii kabla ya kutolewa rasmi na Shirikisho hilo, Alfred aliikanusha ratiba hiyo na kusema kuwa siyo sahihi na kwamba ilikosewa.
“Kwanza niwajulishe kuwa ratiba ambayo ipo kwenye mitandao mbalimbali siyo halisi kwani anwani iliyopo juu imekosewa na tarehe 21 inaonyesha Azam FC watacheza wakati siku hiyo kwenye uwanja huo kutakuwe na mchezo wa Serengeti boys”, alisema Lucas.
 Pia Lucas alisema ratiba ya msimu huu imezingatia mechi za kimataifa za timu za Taifa na Yanga ambayo inashiriki mashindano ya kombe la Shirikisho barani Afrika hivyo haitakuwa na marekebisho na panguapangua za mara kwa mara kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Ratiba ya ligi kuu msimu huu inatarajia kuanza Agosti 20 kwa mechi saba kuchezwa kwenye viwanja tofauti, lakini mchezo wa Yanga na JKT Ruvu utachezwa Agosti 31 kutokana na Yanga kujiandaa na mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe utakaochgezwa Agosti 23.
Kagera Sugar watacheza na Mbeya City Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera, Simba wataikaribisha Ndandsa FC, Uwanja wa Taifa, Toto African watakwaana na Mwadui uwanja wa CCM Kirumba. 
Michezo mingine Stand United dhidi ya Mbao FC, Mtibwa Sugar itawakaribisha Ruvu Shooting, Azam FC wataikaribisha African Lyon Uwanja wa Azam Complex na Majimaji wataikaribisha Tanzania Prison Uwanja wa Majimaji Songea, Ruvuma

*SERIKALI NA BRITISH COUNCIL TANZANIA WAWAPIGA MSASA MASHIRIKISHO YA SANAA NAMNA YA KUANDIKA MAPENDEKEZO YA MRADI WA FURSA YA SANAA YA AFRIKA MASHARIKI

 Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leha Kihimbi (kulia) 
akiwasisitizia baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu umuhimu wa Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge (kulia) akiwaelekeza baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge akiwaelekeza baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.  PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.

*******************************************

SERIKALI kwa kushirikiana na British Council Tanzania imekutana na baadhi ya Viongozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirikisho mbalimbali ya Sanaa nchini na kuwapatia elimu juu ya namna ya kuandika Mapendekezo (Proposals) za Mradi wa kuwania fursa ya sanaa inayodhaminiwa na British Council Tanzania. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE

*BALOZI IDDI AMKABIDHI RIPOTI MIRADI YA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE WA ZANZIBAR BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA

 Balozi wa China, Lu Youqing akipokea Ripoti aliyoiomba  kutoka kwa Balozi Seif Ali Iddi inayofafanua kwa kina mikataba ya miradi ya upanuzi wa sehemu ya Maegesho ya Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ili kusaidia ukamilishaji wa miradi hiyo. Makabidhiano ya Ripoti hiyo yamefanyika Nyumbani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara bara ya Haile Sellasie Jijini Dar es salaam.
 Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China, Lu Youqing aliyepo kati kati akimueleza Balozi  Seif ujio wa Ujumbe wa ngazi ya Juu ya Benki ya Kimataifa ya China ya Exim kwa lengo la kukagua miradi inaqyofadhiliwa na Taasisi hiyo ya Kifedha.
Makamu wa Pili w Rais wa Zanzibar Balozi Seoif (kushoto) akibadilishana mawazo na Balozi wa China Nchini Tanzania, Lu Youqing aliyepo kati kati baada ya kukamilisha mazungumzo yao Jijini Dar es salaam.  Picha na – OMPR – ZNZ.
********************************************************
Ujumbe wa Benki ya Kimataifa ya Jamuhuri ya Watu wa China ya Exim
Bank ukiongozwa na Mkuu wa Benki hiyo unatarajiwa kuwasili Zanzibar
mnamo Tarehe 21 Mwezi huu wa Saba kwa ziara rasmi ya kutembelea miradi
inayofadhiliwa na Taasisi hiyo ya Kifedha ya Nchini China.
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing
alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake Nyumbani kwa Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara Bara ya Haile
Selassie Jijini Dar es salaam kufuatia muendelezo wa mazungumzo yao
kuhusu miradi inayofadhiliwa na Serikali ya China kupitia Benki ya
Exim.
Mazungumzo hayo yamekwenda sambamba na Balozi wa China Bwana Lu
Youqing kupokea Ripoti aliyoiomba kutoka kwa Balozi Seif Ali Iddi
inayofafanua kwa kina mikataba ya miradi ya upanuzi wa sehemu ya
Maegesho ya Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ili
kusaidia ukamilishaji wa miradi hiyo.
Balozi Lu Youqing alisema ujumbe huo wa Benki ya Exim utatembelea na
kuona maendeleo ya ukamilishaji wa ujenzi wa sehemju ya Maegesho ya
Ndege katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amaani Abeid Karume
Kisauni pamoja na kukagua eneo la Mpiga duri linalotarajiwa kujengwa
Bandari ya Kimataifa ya upakizi na ushushaji wa Mizigo.
Balozi Lu alifahamisha kwamba pamoja na ziara hiyo ujumbe huo pia
utafanya mazungumzo ya pamoja na Mawaziri wanaosimamia Wizara za Fedha
na Mipango na Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano na watendani
waandamizi katika jitihada za kuongeza nguvu za kukamilisha miradi
hiyo.
Alisema ripoti aliyoipokea kutoka kwa Balozi Seif itamrahisishia kazi
yake ya ufuatiliaji wa muendelezo wa miradi hiyo na kuelezea faraja
yake kwamba uhusiano kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar
utaendelea kuimarika zaidi kwa karne nyingi ijayo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema Zanzibar inaendelea kuthamini hatua zinazochukuliwa
na Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Benki yake katika kufadhili
miradi mbali mbali ya Maendeleo na Uchumi Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif alisema Jamuhuri ya Watu wa China imeonyesha wazi kuguswa
kwake na harakati za kimaendeleo zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea miundo mbinu imara Wananchi
wake kwenye sekta tofauti zitakazosaidia kuwakwamua kutokana na ukali
wa maisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameipongeza Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Balozi zake za Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla katika kuunga mkono miradi ya Maendeleo ya Wananchi wa
Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi yupo nyumbani kwake Dar es salaam kwa mapumziko
mafupi akiwa njiani kujiandaa kuelekea Mjini Dodoma kuhudhuria vikao
vya juu vya Chama cha Mapinduzi ukiwemo Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa
kumkabidhi Uwenyekiti Rais wa sasa Dr. John Pombe Magufuli.

*WANAWAKE WAFUGA NYUKI KUOKOA MISITU YA PUGU NA KAZIMZUMBWI


Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) Anna Salado na Alicia (kushoto) wakipata maelezo ya fugaji nyuki katika msitu wa hifadhi wa Pugu.
************************************
WANAWAKE wanaofuga nyuki wataokoa hekta 7,270 za misitu ya hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, imefahamika.
Misitu hiyo, ambayo ni miongoni mwa Misitu ya Hifadhi 486 iliyopo nchini, imekuwa hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kijamii hususan uvamizi wa mipaka na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na wananchi mbalimbali.
Meneja wa Misitu hiyo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mathew Mwanuo, anasema kwamba, misitu hiyo iliyopo katika wilaya za Ilala mkoani Dar es Salaam na Kisarawe mkoani Pwani, imekuwa hatarini kutoweka licha ya jitihada za serikali za kukabiliana na wavamizi hao.
“Lakini sasa miradi hii ya ufugaji nyuki inayowahusisha wanawake wa Pugu na Kisarawe itakuwa mkombozi kwa sababu wananchi wenyewe wanahusishwa moja kwa moja na suala la ulinzi,” anasema Mwanuo wakati akiwaelekeza wageni kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka nchini Hispania waliotembelea miradi hiyo hivi karibuni. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Mwanuo anasema kwamba, ndani ya misitu hiyo ya hifadhi kuna jumla ya vikundi vinne vya akinamama vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki wa kisasa, ambapo viwili vinafadhiliwa na mradi wa Green Voices Tanzania na viwili vinafadhiliwa na TFS.
Anna Salado akiwa msituni kuangalia ufugaji wa nyuki kwenye hifadhi ya Pugu.
************************************************
“Kazi ni kubwa katika kuilinda misitu hii, tunao askari wetu wanaozunguka humu, lakini hawatoshi kuweza kuzunguka maeneo yote na ndiyo maana huko nyuma watu walikuwa wakivamia kukata miti na kuchoma mkaa.
“Zamani ulikuwa ukipita pembeni unaona misitu inapendeza, lakini ukiingia ndani kulikuwa na watu wanachoma mkaa huku mambo mengine yakiendelea kama uuzwaji wa vinywaji na kadhalika… yaani hali ilikuwa mbaya sana,” anasema.
Mshiriki kiongozi wa miradi hiyo ya ufugaji wa nyuki chini ya Green Voices, Monica Kagya, anasema kwamba, anaishukuru taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kwa kumwezesha yeye na wenzake 14 kupata mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu ili kuwapa uwezo wanawake kushiriki shughuli za utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mshiriki kiongozi wa mradi wa ufugaji nyuki Pugu na Kazimzumbwi, Monica Kagya, akitoa maelezo kwa wageni (hawapo pichani).
**********************************
“Nilichagua mradi huu wa ufugaji wa nyuki kwa sababu naamini misitu hii ya Pugu na Kazimzumbwi inaweza kuokolewa kutoka katika hatari ya kutoweka, lakini ndiyo mapafu halisi ya Dar es Salaam kwa kuwa inasaidia kutoa hewa ya oksijeni kwenye jiji hilo ambalo idadi ya watu inaongezeka kila siku pamoja na shughuli za uchumi, vikiwemo viwanda,” anasema Kagya.
Bi. Kagya, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa TFS, anasema kwamba, ili kutunza mazingira ni muhimu kuwashirikisha wanawake ambao ndio wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi kutokana na kushughulikia majukumu yote ya nyumbani ikiwemo utafutaji wa nishati za kupikia, hususan kuni na mkaa.
Anasema kwamba, vikundi vyote viwili vinavyotekeleza mradi wa Green Voices vipo katika msitu wa hifadhi wa Pugu ambapo kimoja kina mizinga 12 na kingine kina mizinga 52.
“Vikundi vingine viwili vinavyofadhiliwa na TFS vipo katika msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi,” anasema.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado, ambaye aliwaongoza wenzake kukagua mizinga pamoja na kushuhudia zoezi la urinaji wa asali katika msitu wa Kazimzumbwi, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za kutunza mazingira pamoja na mafanikio ya mradi huo.
“Hakika jitihada hizi ni kubwa, tumefurahi sana kuona akinamama wanakuwa mstari wa mbele kupambana na uharibifu wa mazingira lakini wakati huo huo wanafanya miradi inayoweza kuwakwamua kiuchumi,” alisema Bi. Salado.
 Meneja wa Misitu ya Hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, Mathew Mwanuo, akitoa maelezo na changamoto zinazowakabili.
 Maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika unaofadhili mradi wa Green Voices nchini Tanzania wakiwa wanakaribishwa na wanawake wafuga nyuki katika misitu ya Pugu na Kazimzumbwi kabla ya kuingia msituni kuangalia shughuli za ufugaji huo wa nyuki.
 Alicia (wa pili kulia), mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, akiangalia sega la nyuki katika msitu wa Kazimzumbwi.
Alphonce Matata akiwasha moto kabla ya kuanza shughuli ya urinaji asali.
*************************************
Bi. Salado ameahidi kwamba, katika awamu ya pili ya mradi wa Green Voices, watajitahidi kuwawezesha washiriki katika suala zima la kuongeza uelewa wa madhara ya uharibifu wa mazingira pamoja na kuangalia uwezekano wa kutatua changamoto zinazowakabili, zikiwemo za vitendea kazi kama mavazi pamoja na mizinga ya kutosha.
Mradi wa Green Voices unatekelezwa nchini Tanzania pekee chini ya ufadhili wa WAF na ulizinduliwa jijini Dar es Salaam Julai 11, 2016 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa sambamba na rais wa taasisi ya WAF ambaye pia ni makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria Teresa Fernandez e la Vega, ambaye tayari amekwisharejea jijini Madrid.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amepongeza jitihada za akinamama hao na kuwataka wawe walimu wa jamii nzima ili kuokoa misitu hiyo.
Bi. Secelela, ambaye ni mwanahabari kitaaluma, amesema kwamba, walau hali sasa inaonyesha kubadilika kuliko ilivyokuwa siku za nyuma ambapo misitu hiyo ilikuwa inakaribia kutoweka.
“Nilikuja huku miaka mitano iliyopita wakati nikiandika habari za mazingira, hali ilikuwa mbaya sana, maana katikati yam situ nasikia kuna watu waliweka mpaka baa, lakini sasa kwa kuanzisha miradi hii ambayo inawataka wanamradi kuzungukia kila wakati kwenye mizinga yao kutawakimbiza wavamizi wote,” alisema.
Ameongeza kwamba, uwepo wa misitu hiyo ni muhimu kwa sababu ndiyo ‘mapafu ya Dar es Salaam’ katika kukabiliana na hewa chafu inayozalishwa jijini humo.

*DC MTATURU AKUTANA NA WAZEE WA WILAYA YA IKUNGI AWAAHIDI KUFANYA KAZI KWA BIDII

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji J. Mtaturu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wazee waliowawakilisha wazee wengine wilayani humo
Dc Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa kikao. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Mtaturu akisikiliza kwa makini moja ya ushauri uliopatiwa na wazee baada ya kikao kumalizika
******************************************
Na Mathias Canal, Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu amekutana na zaidi ya wazee 137 kutoka vijiji 101 vilivyopo katika Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida. Katika mazungumzo ya mkuu huyo wa Wilaya na wazee hao yalijikita zaidi katika kujadili namna ya kukabiliana na umasikini kupitia nguvu Kazi ya Taifa (Vijana) katika kilimo na ufugaji wa kisasa. 

Dc Mtaturu amewasilisha dhamira ya serikali ya Hapa Kazi Tu chini ya Rais wa Awamu ya Tano Dkt John Joseph Pombe Magufulu kwa wazee wa Wilaya ya Ikungi na Taifa kwa ujumla ni kupambana na mafisadi, Rushwa na wahujumu uchumi ili kuboresha huduma za Jamii ikiwemo Afya hususani katika kuboresha huduma za Afya kwa wazee wote nchini sawia na Wanawake wajawazito na watoto. 
Katika kuhakikisha kunakuwa na chachu ya maendeleo kwaMapinduzikubwa Wilayani humo Mtaturu alisema kuwa serikali imekusudia kuboresha kilimo na ufugaji ili viwe vya tija na kibiashara na kupelekea kupunguza umasikini wa wananchi mwaka hadi mwaka. 
Mtaturu anakuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza kukutana na kundi la wazee Siku chache baada ya kuapishwa jambo ambalo halijawahi kutokea kwa kiongozi mwingine yeyote Wilayani humo tangu Mkoa wa Singida ulipoanzishwa. 
Kwa upande wao wazee hao wameonyesha wazi mapenzi yao ya dhati kwa mkuu huyo wa Wilaya na kuahidi ushirikiano uliotukuka katika utendaji wake. Wakati huo huo wazee hao wamemshukuru Mh Rais Magufuli kwa uteuzi alioufanya kumpeleka Mkuu huyo wa Wilaya kuongoza wananchi hao ambao wameonyesha kukatishwa tamaa na baadhi ya viongozi wa serikali wilayani humo ambao wameshindwa kutatua changamoto za wananchi. 

Awali Dc Mtaturu alikuwa na kikao cha mapema na watumishi wa Halmashauri na wakuu wa idara ili kukumbushana majukumu ya kila mmoja utendaji wake na kuwasihi kufanya Kazi kwa bidii zaidi kwa kushirikiana na wananchi. Mtaturu amewakumbusha watumishi hao wajibu wao wa kusimamia miradi ya maendeleo kwa kupata thamani halisi ya fedha (Value for Money) kushughulika na kero za wananchi ikiwemo kutafsiri ilani ya Uchaguzi kwa vitendo ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewapa muda wa mwezi mmoja watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wanaoishi Singida Mjini takribani kilomita 41 kutoka Wilayani hapo wawe wamehamia Wilayani Ikungi kwani amebaini ni watumishi wanne pekee ndio wanaoishi Wilayani hapa jambo ambalo linapunguza ufanisi wa Kazi. 

Katika sekta ya michezo Mtaturu alisema kuwa ili kuibua vipaji na Mkoa wa Singida kwa muda mrefu umekuwa na Sifa ya kutoa wanariadha hivyo ili kuenzi heshima hiyo anataraji kuanzisha Ikungi Marathon ili kuwapa fursa Vijana wenye vipaji kuibuka na kufika mbali zaidi katika medani za riadha