Mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (katikati) akiwatoka mabeki wa Moeocco, wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, uliochezwa jana usiku Jijini Marakech, Morocco. Katika mchezo huo Morocco walishinda mabao 2-1.
Mshambuliaji wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu (kulia) akimtoka mabeki wa Moeocco, wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, uliochezwa jana usiku Jijini Marakech, Morocco. Katika mchezo huo Morocco walishinda mabao 2-1. Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry
*******************************
Na Boniface Wambura,Marrakech
Taifa Stars imepoteza mechi ya ugenini baada ya kufungwa mabao 2-1. Mechi hiyo ya kundi C ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil dhidi ya Morocco imechezwa jana (Juni 8 mwaka huu) usiku kwenye uga wa Grand Stade de Marrakech, jijini Marrakech.
Licha ya kufungwa, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumjaribu kipa wa Morocco, Nadir Lamyaghri aliyeokoa shuti la mpira wa adhabu la Aggrey Morris katika sekunde ya 40 tu tangu refa Daniel Frazier Bennett kutoka Afrika Kusini apulize filimbi ya kuanzisha pambano hilo.
Refa alitoa faulo hiyo baada ya mshambuliaji Thomas Ulimwengu kukwatuliwa na Ahmed Kantari baada ya kumtambuka beki mwingine wa Simba hao wa milima ya Atlas.
Stars walicheza pungufu kwa dakika 58 baada ya Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumkwatua ndani ya eneo la hatari Abdelaziz Barrada huku akiwa amebaki yeye na mshambuliaji huyo. Adhabu hiyo iliandamana na penati ambayo Morocco waliitumia kupata bao la kuongoza dakika ya 37 mfungaji akiwa Abderazzak Hamed Allah.
Kabla, Stars wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager walitengeneza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 25 baada ya Ulimwengu kufanikiwa kuwatoka mabeki wawili wa Morocco na kuingia eneo la hatari lakini shuti lake hafifu lilidakwa na kipa Lamyaghri.
Morocco waliongeza bao lingine dakika ya 50 na Youssef El Arabi baada ya mabeki wa Stars kujichanganya katika kudhibiti pasi ya mwisho ya wachezaji wa timu hiyo, na mshambuliaji huyo kumfunga kirahisi kipa Juma Kaseja.
Kiungo mshambuliaji Amri Kiemba aliifungia Stars bao maridadi dakika ya 61 kwa mkwaju wa mbali uliomshinda kipa Lamyaghri. Kabla ya kuachia shuti hilo, Kiemba aliwatoka wachezaji wa timu ya Morocco ambayo ndiyo imepeta ushindi wake wa kwanza katika mechi hizo za mchujo za Kombe la Dunia.
Dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho Mbwana Samata angeweza kuisawazishia Stars, lakini licha ya kuwatoka mabeki wawili wa Morocco baada ya kupokea pasi ya John Bocco mpira aliopiga ulitoka nje.
Stars ambayo bado inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi sita inaondoka hapa kesho (Juni 9 mwaka huu) mchana kwa ndege ya EgyptAir kupitia Cairo, Misri na itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 alifajiri (Juni 10 mwaka huu).
Katika mechi hiyo Stars iliwakilishwa na; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa/Nadir Haroub, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha/John Bocco, Amri Kiemba na Mbwana Samata
No comments:
Post a Comment