Tanzania imeanza Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) inayofanyika nchini Botswana kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mali kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 katika mechi iliyochezwa leo (Mei 22 mwaka huu).
Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa SSKB jijini Gaborone ambapo Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 52 mfungaji akiwa Amani Ali. Hata hivyo, Mali walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 61.
Tanzania itacheza mechi yake ya pili kesho (Mei 23 mwaka huu) kwa kuwakabili wenyeji Botswana kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 8 kamili mchana kwa saa za Tanzania. Mechi hizo zinaoneshwa moja kwa moja na kituo cha SuperSport.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Tanzania itacheza mechi nyingine Mei 25 mwaka huu dhidi ya Swaziland, itakuwa tena uwanjani Mei 27 mwaka huu kuikabili Nigeria wakati mechi ya mwisho itakuwa Mei 29 mwaka huu dhidi ya Afrika Kusini.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment