Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mwakilishi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika Mkutano Mkuu wa TFF, William Chibura kilichotokea leo asubuhi (Juni 3 mwaka huu) katika Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini Musoma.
Chibura aliyezaliwa mwaka 1969 alikuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Mara kupitia FAM. Aliwahi kuichezea Musoma Shooting, na baadaye kuwa kiongozi katika klabu hiyo na ile ya Polisi Mara iliyoko Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Hadi mauti yanamkuta alikuwa kiongozi wa Butiama FC, na mwakilishi wa klabu Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Butiama (MUFA) kwenye Mkutano Mkuu wa FAM.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini kwani, Chibura enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa katika mchezo huu tangu akiwa mchezaji na baadaye kiongozi.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Chibura, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Jeshi la Polisi Tanzania na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania- Mkoa wa Mara, kwani marehemu Chibura alikuwa mtumishi wa jeshi hilo. TFF tunasubiri taratibu hizo ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo.
Bwana alitoa, na Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina
No comments:
Post a Comment