Monday, March 31, 2014

WANANCHI WATAKIWA KUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO


Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia bi Prisca Ulomi akitoa wito kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  wakati wa mkutano  na waandishi wa habari leo jijini Dar es salam.
Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Bi Prisca Ulomi akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hatua iliyofikiwa na Serikali katika  Uandaaji wa Sheria ya Matumizi Salama ya Mtandao,kushoto ni Afisa habari wa Idara ya Habari Maelezo Bi Fatma Salum. 
*****************************************
Fatma Salum-Maelezo
Serikali yawatahadharisha wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuondoa vitendo vya uhalifu hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi Prisca Ulomi wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Bi Prisca amesema kuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa kutambua umuhimu wa TEHAMA wameamua kuandaa muswada wa Sheria  za Matumizi Sahihi na Salama ya Mtandao (Cyber Laws).

Akieleza zaidi Bi Prisca amesema kuwa Muswada wa sheria hizo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi (The Personal Data Protection Bill), Muswada wa Sheria ya Biashara ya Miamala ya Kielektroniki (Electronic  Transaction Bill), na Muswada wa Sheria ya Kuzuia Uhalifu kwa njia ya Kompyuta na Mtandao (Computer and Cyber Crimes Bills).

“Sheria hizo zitasaidia kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hapa nchini kwa kudhibiti uhalifu kwa kutumia mitandao na kuwalinda watoto dhidi ya matumizi yasiyofaa ya mitandao”. alisema Bi Prisca.
Bi Prisca aliongeza kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuweka miundombinu ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha na kuharakisha utoaji wa huduma mbalimbali na kubainisha kuwa wapo baadhi ya watu wanatumia vibaya teknolojia hiyo, hivyo kuna umuhimu wa kuwepo sheria zitakazodhibiti uhalifu kupitia mitandao.

Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia  imetoa rai kwa wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao na badala yake watumie vizuri mitandao hiyo kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla hali inayoweza kuathiri ukuaji wa sekta hiyo nchini

No comments:

Post a Comment