Sunday, May 25, 2014

BALOZI SEIF IDDI AKABIDHI KOMBE KWA TIMU SOKA YA CHUKWANI UNITED.


 Timu za Chukwani United iliyovalia jezi rangi nyekundu na New Generation zikimenyana ndani ya dimba la Kiembe samaki katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano ambapo chukwani United ilitawadhwa kuwa bingwa wa kombe hilo kwa kuichakaza New Generation goli 2-0 Mgeni rasmi akiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi.

 Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo akifafanua mpangilio wa zawadi zitakavyotolewa kwa washindi na washiriki wa Kombe la Muungano lililoandaliwa ndani ya Jimbo hilo.
Kushoto yake ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na pembeni yake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mahindano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Kikombe pamoja na baadhi ya zawadi Kepteni wa Timu ya Soka ya Chukwani United Mohd Golo baada ya Timu yake kushinda mchezo wa Fainal kwa goli 2-0 dhidi ya New Generation.
Wachezaji wa timu ya soka ya Chukwani United wakishangiria ushindi wao dhidi ya Timu ya New Generation iliyoupata wa Goli 2-0 kwenye mchezo wa fainali wa mashindano ya Kombe la Muungano lililoandaliwa ndani ya Jimbo la Kiembe Samaki.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Press Release:-                 { Michezo }
Hatimae Bingwa wa Mashindano ya Kombe ya Muungano yaliyoanza kutimua vumbi tarehe 23 April Mwaka huu na kushirikisha Timu za Soka zipatazo Kumi na Moja za Jimbo la Kiembe Samaki Wilaya ya Magharibi  amepatikana na kufikia hatma yake kwenye uwanja wa michezo wa Kiembe Samaki.
Chukwani United ilitawadhwa kuwa bingwa wa kombe hilo baada ya kuikung’uta New Generation ya Kiembe samaki kwa Magoli mawili kwa bila kwenye pambano la fainali ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika na mamia ya wapenzi wa mchezo wa soka walioshuhudia pambano hilo kali na la kuvutia.
Magoli yote mawili ya Timu ya Soka ya Chukwani United yaliwekwa kimiani katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambapo Goli la kwanza  lilifungwa na mchezaji Khatib Abdulla lile la pili likafungwa na Mfaume Abdulla.
Mchezo huo wa fainali uliweza kuleta burdani safi kwa wapenzi wa soka huku wakishuhudia kasi na ufundi wa soka ulioonyeshwa na Vijana hao wa pande zote mbili.
Hadi dakika tisini za mchezo huo wa fainali zinamalizika Chukwani United ilitoka uwanjani kifua mbele kwa kupata magoli hayo mbili na New Generation hawakupata kitu.
Akizungumza mara baada ya pambano hilo mgeni rasmi wa fainali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza vijana hao pamoja na Uongozi wa Jimbo la Kiembe Samaki kwa uamuzi wao wa kuandaa na kushiriki kwenye mashindano hayo kwa njia ya amani na salama.
Balozi Seif alisema mchezo wa soka hivi sasa umekuwa ukitoa ajira kubwa Kitaifa na Kimataifa. Hivyo aliwaasa Vijana hao kuendelea kufanya bidii katika kudumisha mchezo huo ili hapo baadaye mchezo huo usaidie fursa nzuri ya kuwaendeshea maisha yao.
“ Wengi kati yenu mnatamani kuwa kama George Wheah,Tierry Henry, Ronaldinho au Messi na ndoto hiyo mnaweza kuifikia endapo mtajikita zaidi katika kudumisha mazoezi ya nguvu na nidhamu “. Alisema Balozi Seif.
Katika kuunga mkono juhudi za Vijana hao wa Jimbo la Kiembe samaki za kuendeleza Mchezo wa Soka Balozi Seif amekubaliana na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahomud Thabit Kombo kuunda udugu wa kimichezo kati ya Vijana wa Majimbo hayo mawili.
Alisema mipango itafanywa hapo baadaye ya kuandaa mashindano ya mchezo utakayojumuisha pamoja wachezaji wa Majimbo yote mawili lengo likiwa kuimarisha urafiki na kujenga udugu wa pande hizo mbili kimichezo.
Akizungumzia suala la Amani na usalama wa Nchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaasa vijana hao kujiepusha na vishawishi vinavyoonekana kufanywa na baadhi ya watu hasa wana siasa katika kuichezea amani iliyopo hivi sasa.
Alisema hali ya amani iliyopo nchini ndio njia ya msingi iliyowapa fursa vijana hao kuendeleza mchezo wa soka sambamba na jamii kushughulikia harakati zao za kutafuta riziki katika maeneo tofauti.
“ Vijana lazima mfikie pahali na kukubali kuwa wadau wakubwa wa amani iliyopo nchini na kukataa kurubuniwa na watu wenye tabia ya kutaka kuona shari inatawala wakati wote katika maeneo mbali mbali nchini “. Alifafanua Balozi Seif.
Katika Fainali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi zawadi mbali mbali kwa washindi wa mashindano ya kombe hilo la Muungano zilizotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki sambamba na yeye binafsi kuongeza zawadi ya mipira miwili kwa kila Timu iliyoshiriki mashindano hayo kati ya timu 11.
Zawadi hizo zilikuwa ni pamoja na Timu shiriki zote kupata fedha taslimu, mshindi wa tatu, mshindi wa pili na mshindi wa kwanza kupewa fedha taslim pamoja na vikombe.
Halkadhalika Kipa Bora, waamuzi wa mashindano hayo, timu yenye nidhamu, mfungaji bora sambamba na Tawi la CCM Kiembe samaki na Maskani ya Kisima Mbaazi zikazawadiwa Seti ya TV na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki kuanza kutekeleza ahadi aliyowapa.
Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo ambae ndie aliyedhamini michezo hiyo alisema Uongozi wa Jimbo hilo ulifikia hatua ya kuandaa mashindano hayo ya kombe la Muungano ili kupata mapumziko mazuri ya bunge Maalum la Katiba lililokuwa likiendelea Mjini Dodoma.
Mahmoud alisema lengo la kuandaliwa kwa mashindano hayo ni kudumisha Muungano, kulinda umoja na Mshikamano miongoni mwa wananchi na hasa vijana wa Jimbo hilo.
Jumla ya shilingi Milioni 5,500,000/- zimetumika katika kuandaa mashindano hayo yaliyoanza Tarehe 23 April mwaka 2014 na kushirikisha timu 11 za Jimbo  zima la Kiembe samaki zikiwa katika  makundi mawili kwenye viwanja vya Kiembe Samaki, Mbweni pamoja na Chukwani.
Timu hizo ni pamoja na Hebron, Buyu, Kiembe Samaki, Mbweni Star, Mbweni Kids, New Boys, New  Generation, Small Ziko, Mbweni Academy, Kisima Mbaazi pamoja na Mabingwa wa mashindano hayo Chukwani United.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
25/5/2014.

No comments:

Post a Comment