Tuesday, May 28, 2013

*KAMPUNI YA INTELLECTUALS YAZIOMBA KAMPUNI NYINGINE KUJITOKEZA KUDHAMINI UHURU MARATHON


 Mkurugenzi wa Kampuni ya Intellectuals ambao ndiyo waandaaji wa mbio hizo, Innocent Melleck akiongea katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa wadhamini wa Uhuru Marathon iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu mkuu wa Chama Cha Riadha Tanzania, Seleman Nyambui.
 Katibu mkuu wa Chama Cha Riadha Tanzania, Seleman Nyambui, akizungumza na  waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa wadhamini wa Uhuru Marathon iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya  Intellectuals ambao ndiyo waandaaji wa mbio hizo, Innocent Melleck 
Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano huo wakiwajibika  wakati wa ufunguzi wa wadhamini wa Uhuru Marathon iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
***********************************
Na Mwandishi Wetu
WAKATI mbio zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na watu wengi hapa nchini za Uhuru Marathon zikitarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu, waratibu wa mbio hizo wamezitaka kampuni, taasisi au watu binafasi wanaotaka kuzidhamini wafanye hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Intellectuals walio waandaaji wa mbio hizo, Innocent Melleck alisema wameamua kufungua milango ya udhamini, ili ziweze kufana zaidi.
Melleck alisema, wanariadha wengi kutoka ndani na nje ya nchi wameonyesha nia ya kushiriki mbio hizo zitakazokuwa zikifanyika kila Desemba zikiambatana na maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara, hivyo wameona ni bora wafungue milango kwa wadhamini.
“Nadhani wote mnakumbuka uzinduzi wa mbio hizi za Uhuru, uliofanyika Desemba mwaka Jana, ukiwa unaashiria kuanza kwa mchakato wa maandalizi ya mbio zenyewe ambazo zitaanza kufanyika Desemba mwaka huu.
“Mbio hizi za Uhuru, kama lilivyo jina lake zimeanzishwa ili kuongeza chachu kwa Watanzania kuwa na moyo wa kulinda amani, umoja na mshikamano wetu.
“Kwa sasa maandalizi ya awali yanaendelea vizuri, nasi tumeona huu ni muda muafaka kufungua milango ya udhamini kwa makampuni, mashirika na taasisi mbalimbali ambazo zitahitaji kushirikiana nasi katika kufanikisha mbio hizi wajitokeze na kupata taratibu za udhamini,” alisema Melleck.
Alisema kutakuwa na mbio ndefu za kilomita 42, mbio za kati za kilomita 21 na zile za kujifurahisha za kilomita 5, hivyo mdhamini anaweza kuchagua aina ya mbio anazotaka kuzidhamini.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui alisema, tayari kwa upande wao wamekamilisha vitu vingi ikiwemo kupendekeza mzunguko wa mbio hizo na kuangalia mambo yote ya kiufundi.
“Tunawaomba wadhamini wajitokeze ili kwa pamoja tuweze kufanikisha mbio hizi zenye malengo mazuri kwa Taifa letu kwa ujumla.
“Mbio hizi tutazisimamia na kuziendesha katika hadhi ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa zaidi ya kulinda Amani na Umoja wetu, pia tunalitangaza taifa letu kote ulimwenguni.
“Kwa kuwa mimi ninaangalia zaidi upande wa ufundi, nichukue nafasi hii pia kuwasihi wanariadha wa hapa nchini kuanza maandalizi ya mbio hizi, itakuwa si vyema nafasi za juu zikichukuliwa na wageni, wakati sisi tunao wanariadha wazuri hapa nyumbani,” alisema.
Uhuru Marathon ni moja kati ya mbio zinazotarajiwa kuleta mapinduzi mapya katika riadha, ikiwa pamoja na kukumbusha umuhimu wa kutunza na kulinda amani tuliyonayo.

No comments:

Post a Comment