Thursday, May 30, 2013

*MASHINDANO YA KUMRITHI REDD'S MISS TANZANIA, BRIGIT KUENDELEA LEO


Na Mwandishi Wetu
KINYANG’ANYIRO cha safari ya kumpata Redd’s Miss Tanzania, kinazidi kushika kasi ambapo leo kutakuwa na mashindano katika vitongoji kadhaa vya kupata warembo wao.
Kazi kubwa itakuwa ya kumsaka Redd’s Miss Tabata, shindano ambalo linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Dar West Park uliopo Tabata, pale warembo watakapopanda jukwaani kumsaka yule atakayetwaa taji.
Kwa mujibu wa Mratibu wa shindano hilo, Joseph Kapinga kila kitu kimekamilika, huku burudani ikitarajiwa kutolewa na bendi ya African Stars  ‘Twanga Pepeta’ na katika ukumbi wa Club Bilcanas kutakuwa na kinyang’anyiro cha wasomi wa vyuo vikuu mbalimbali toka eneo la Temeke ambao watamsaka mrembo wao hapo na burudani itaongozwa na Ben paul huku kiingilio kikiwa sh 10,000  .
Wakati Tabata wakisaka mrembo wao, shughuli pevu itakuwa katika Ukumbi wa Kilimani, Dodoma kumsaka Redd’s Miss Dodoma, wakati warembo zaidi ya 10 watakapopanda jukwaani.
Katika shindano hilo litakalokuwa na burudani kadhaa kutoka kwa Richie Mavoko na Saki Band, kiingilio kinatarajiwa kuwa Sh 20,000 kwa viti maalumu na Sh 10,000 kwa vilivyobaki.
Redd’s Miss Singida naye anatarajiwa kupatikana leo katika shindano linalotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge.
Katika shindano hilo pia kutakuwa na burudani kadhaa zitakazotolewa na Mzee Majuto, Mpoki na Ally Nipishe. Pia kutakuwa na shindano la Redd’s Miss Njiro, linalotarajiwa kufanyika leo.
Kinyang’anyiro cha kusaka warembo kinatarajiwa kuendelea kesho, ambapo kutakuwa na shindano la Redd’s Miss Dar City Centre, Redd’s Miss Mtwara, Redd’s Miss Pwani, Redd’s Miss Geita, Redd’s Miss Manyara na Redd’s Miss Rukwa.

Shindano la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments:

Post a Comment