Wednesday, April 9, 2014

AFRICAN STARS 'TWANGA PEPETA' WAINGIA MKATABA NA KAMPUNI YA PROIN PROMOTIONS KUANDAA KAZI ZAO



 Na: Sufianimafoto Reporter, Dar 
BENDI ya muziki wa dansi nchini ya African Stars 'Twanga Pepeta',
wameingia mkataba maalumu na kampuni ya Proin Promotions 
Limited kwa ajili ya utengenezaji wa kazi zao. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, 
Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, alisema mkataba 
huo una manufaa kwa bendi hiyo kutokana na kutaka kuwanufaisha wanamuziki na wasanii wa nchini kwa ujumla. 

Baraka alisema kampuni hiyo ambayo awali ilikuwa 
ikijishughulisha na usambazaji wa kazi za filamu, imeamua kuingia mkataba na bendi yake kutokana na ubora wao. 

Alisema wasanii nchini wanatakiwa kunufaika na kazi
  wanayoifanya, na Prain wameihakikishia Twanga kuwa kazi zao 
sasa zimetengenezwa kwa ubora wa hali ya juu kiasi cha 
kumshinda mtu yeyote kuirudufu.

 "Tunataka maendeleo ya wasanii, tumekuwa tukiwakumbatia 
zaidi wasanii wa nje, lakini muunganiko wetu sasa utasaidia kuinua hali ya kipato sahihi kwa wanamuziki tulionao," alisema Baraka. 

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Prain Promotions, Evance 
Steven, alisema kampuni yao imeamua kuingia kwenye muziki na 
kuichagua Twanga Pepeta kuwa bendi ya kwanza kutokana na 
kazi yao wanayofanya katika burudani.

 Steven alisema kazi kubwa waliyoanza nayo katika albamu ya 
Twanga Pepeta ya Dunia Daraja ni kuhakikisha kuwa haiwezi 
kunakiliwa (kurudufiwa) upya na maharamia wa kazi za kisanii 
nchini kama ilivyozoeleka.

 "Tumewahakikishia wenzetu wa Twanga Pepeta kuwa kazi zao 
sasa ziko salama kuuzwa kihalali kutokana na kuziwekea programu maalumu ya kushindwa kunakilika, hivyo kila mtu atanunua kihalali kazi za bendi hii za Dunia Daraja," alisema ofisa huyo. 

Twanga itaanza kuuza kazi hizo katika kila maonesho yao huku zikionekana kufungwa katika ubora wa hali ya juu alipokuwa akiwaonesha waandishi wa habari utofauti mkubwa uliofanywa na Prain, ambapo pia zina stika maalumu za TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania).

No comments:

Post a Comment