Katibu Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. Adam Mambi akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu Mpango wa kuanza utafiti katika mapitio ya mfumo wa sheria unaosimamia haki za walaji ikiwa ni hatua mojawapo katika mchakato wa kuundaa sheria inayowalinda watumiaji wa huduma mbalimbali hapa nchini. Kulia ni Afisa Sheria wa Tume hiyo ni Fred Kandonga.
Afisa Sheria wa wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Fred Kandonga akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu sababu zilizopelekea Serikali kuamua kufanya utafiti utakaopelekea kutungwa kwa sheria itakayosaidia kuwepo kwa mfumo wa biashara wenye uwiano katika ushindani. Katikati ni Katibu Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. Adam Mambi, anayemfuatia ni Afisa Habari Idara ya Habari Maelezo Frank Mvungi na Mwisho kushoto ni Afisa habari wa Tume hiyo Munir Shemweta.
************************************
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TUME YAANZA UTAFITI KATIKA MAPITIO YA MFUMO WA SHERIA UNAOSIMAMIA HAKI ZA WALAJI
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza kufanya utafiti wa mfumo wa sheria unaosimamia Haki za Walaji ili kubaini kasoro mbalimbali zilizoko kwenye mfumo husika na kupendekeza njia sahihi ya kuboresha mfumo huo nchini Tanzania.
Hatua ya Tume kufanya utafiti huo inatokana na mendeleo ya sayansi, teknolojia pamoja na utandawazi ambayo kwa ujumla yamemfanya mlaji kujikuta akiwa kwenye hatari ya kuathirika kiafya, kiuchumi na kijamii.
Tume katika utafiti wa awali, imebaini kuwa Mfumo uliopo hauendani na na wakati huu wa mabadiliko ya kiuchumi, kijsamii, kitekenologia yanayotokea, kwani sheria nyingi zilizopo zilitungwa muda mrefu na hivyo hazikuzingatia mahitaji ya wakati wa sasa.
Pia sheria nyingi hazijajumuishwa kwenye sheria moja zinasimamiwa na watu au Taasisi tofauti tofauti. Hivyo, Tume imeona haja ya kupitia sheria hizo ili kupendekeza mfumo wa sheria utakaomlinda mlaji kwa kuzingatia maendeleo yaliyopo sasa.
Na ni matarajio yetu baada ya kukamilika kwa utafiti huu Tume tutakuja na mapendekezo ambayo yataleta tija kwa walaji wetu pamoja na taifa kwa ujumla.
Tume ya Kurekebisha Sheria (Tume) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kurekebisha Sheria Namba 11 ya mwaka 1980. Sheria hii kwa sasa ni Sura ya 171 ya Sheria za Tanzania Toleo la Mwaka 2002. Tume ya Kurekebisha Sheria ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Imetolewa na;
Tume ya Kurekebisha Sheria (T)
Dar es Salaam
04 Aprili, 2014
No comments:
Post a Comment