Wednesday, June 19, 2013

*MAMA SALMA KIKWETE APONGEZWA KWA KUENDELEZA SOKA NCHINI


Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amepongezwa kwa jitihada zake za kuinua sekta ya michezo nchini   jambo ambalo limewafanya  vijana wengi kujipata ajira katika fani hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Lindi  (LIREFA) Francis Ndulane wakati wachezaji wa timu ya Kariakoo ya mkoa huo walipozitembelea ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)  zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ndulane alisema kuwa mchango unaotolewa na  Mama Kikwete umewapa hari na kuwatia  moyo vijana wengi na hivyo kuweza kuendeleza sekta ya michezo mkoani humo.
Alisema kuwa hapa nchini vijana wengi wana vipaji mbalimbali, lakini hawana watu wa kuwaendeleza, hivyo alimshukuru kwa jitihada zake za kuwaendeleza katika sekta hiyo na hivi sasa  wanaamini  kuwa wataweza kujiajiri na kuweza kuzisaidia familia zao.
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA aliwapongeza wachezaji hao kwa juhudi kubwa wanayoifanya katika soka hadi kufikia hatua ya kushiriki ligi ya taifa ya mabingwa wa mkoa ngazi ya taifa na kufikia hatua ya nane bora.
Naye Mwenyekiti wa timu hiyo Abdalah Livemba aliwashukuru Mama Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kwa moyo walionao wa kuisaidia timu hiyo hadi kufikia  hapo ilipo.
Alimuomba kuwatafutia mdhamini ili awezkuwasaidia  kubeba mzigo mkubwa wa kuitunza timu hiyo ambao unaelekea kuwalemea.
Mama Kikwete aliikabidhi timu hiyo zawadi za  viatu pea 29, jezi seti mbili ambazo ni 32, mipira mitatu, pampu moja na  soksi  pea 16.
Timu ya Kariakoo inashiriki mashindano ya ligi ya mabingwa mkoa ngazi ya Taifa ambayo yalianza tarehe 12/6/2013 kwa kuzishirikisha  timu 28 kutoka nchi nzima wao wamebaki kati ya timu nane na leo wanapambana na Friends Rangers ya mkoa wa Dar es Salaam mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment