Sunday, June 23, 2013

*MWIGULU NCHEMBA NA PETER MSIGWA NUSURA WAZICHAPE 'KAVU KAVU' DODOMA


Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akizozana na wabunge wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa(kulia)mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (wa pili kulia) na Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (wa pili kushoto) baada ya kukutana nje ya ukumbi wa mikutano wa St Gasper,Dodoma jana wakati wa semina ya wabunge ya kuhusu Ukimwi. Picha na Fidelis Felix 
*******************************************
*Tukio hilo lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma, walipokwenda kwa ajili ya kuhudhuria semina ya wabunge wapambanaji na Ukimwi, ambapo baadhi ya wabunge wa Chadema walihudhuria, baada ya kutoonekana mjini humo tangu Juni 17 mwaka huu.

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba jana nusura wachapane makonde baada ya kutupiana maneno ya kashfa, wakituhumiana kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea Jumamosi iliyopita mkoani Arusha.
Tukio hilo lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma, walipokwenda kwa ajili ya kuhudhuria semina ya wabunge wapambanaji na Ukimwi, ambapo baadhi ya wabunge wa Chadema walihudhuria, baada ya kutoonekana mjini humo tangu Juni 17 mwaka huu.
Wabunge hao wa Chadema hawakuhudhuria kikao chochote cha Bunge kutokana na kwenda mkoani Arusha kwa shughuli mbalimbali, kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wao wa kuhitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika viwanja vya Soweto, Juni 16 jijini humo.
Malumbano hayo yanatokana na Nchemba kuituhumu Chadema kuhusika na mlipuko huo, Juni 20 mwaka huu wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema chama hicho kilipanga kulipua bomu hilo ili kuwafanya Watanzania waamini kuwa Serikali ya CCM ndiyo inayohusika na tukio hilo.
TUKIO LILIVYOANZA:- Wakati Msigwa akiingia katika ukumbi huo akiwa ameongozana na Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje, walikutana uso kwa uso na Nchemba ambaye alikuwa akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Amour Arfi.
Baada ya Nchemba kumwona Msigwa alimkaribisha mchungaji huyo akisema; “Karibu sana bwana, salama lakini?”
Hata hivyo, badala ya kujibu salamu hiyo ya Nchemba, Msigwa alikuja juu na kumtuhumu Nchemba kwamba anatoa kauli zinazoweza kuvuruga amani ya nchi.
“Wewe ni mtu hatari sana, haya yote yanasababishwa na wewe, mnatumia damu za watu kutafuta madaraka,” alisema Msigwa akimtupia maneno Mwigulu.
Baada ya kauli hiyo Nchemba alihoji akisema: “Ki-vipi? Hayo mambo tuyaache, Msigwa achana na haya mambo!”
Baada ya Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM kujibu, Msigwa alimsogelea karibu na kumnyooshea kidole, huku akiendelea kumtuhumu kuwa ana siasa chafu zinazopandikiza chuki kwa jamii.
Malumbano hayo pia yaliingiliwa na Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere ambaye alimuunga mkono Msigwa, huku akimtuhumu Nchemba kuwa ni mtu mbaya katika siasa za Tanzania. Katika kile kilichoonekana kutaka kuweka mambo sawa, Wenje alimvuta Msigwa na kumpeleka ukumbini ili kuepusha shari baada ya wabunge hao kuzidi kurushiana maneno. Chanzo:- www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment