Tuesday, June 25, 2013

*WANAWAKE WANA UWEZO WA KUBADILISHA MAISHA YA MTANZANIA


Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa akitoa hotuba yake  wakati wa ufunguzi  wa mafunzo ya siku tatu ya wanawake wajasiriamali yanayoendelea kwenye  ukumbi wa Bwalo la Maafisa la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Mgulani jijini Dar es salaam.
***************************************
NA BELINDA KWEKA – MAELEZO
WANAWAKE wakiwezeshwa kiuchumi na kupatiwa elimu ya msingi ya ujasiriamali, kuepuka maradhi hatarishi na kufahamu haki zao katika jamii, umasikini utapungua,  kipato  kitaongezeka na maisha ya Watanzania yatabadilika. 
 Hayo  yalisemwa leo na Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa wakati wa ufunguzi  wa mafunzo ya siku tatu ya  wanawake wajasiriamali yanayoendelea kwenye  ukumbi wa Bwalo la Maafisa la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Mgulani jijini Dar es salaam.

Mama Anna Mkapa ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa   alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii  wajasiriamali  hao kutoka mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani, ambapo jumla ya wanawake wapatao 264 wanashiriki.

“Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote umekusudia kwa nguvu zake zote kuendeleza vita ya hii ya kuwawezesha wanawake  nchini  kujikwamua katika wimbi la umasikini, maradhi na ujinga,” alisisitiza Mama Mkapa.
 Aidha ameiomba Serikali, Asasi za kiraia, taasisi za dini, wahisani binfasi ndani na nje ya nchi, kusaidia  wanawke haswa wa vijijini   kujikwamua na umasikini. 

 Mama Mkapa  aliongeza  kuwa mfuko huo, kwa kipindi cha miaka 16  zaidi ya wanawake 6,820 wamepata mafunzo ya stadi za biashara na wengine  4,500 wamepata fursa ya kushiriki maonyesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa kupitia EOTF ili  kutangaza na kuuza bidhaa zao.

 Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Dk. Abdallah Kigoda  akifungua mafunzo hayo alisema  Serikali imeanzisha utaratibu wa kuweka kumbukumbu za mkopo katika mabenki kwa kupitia ‘Credit Reference Bureau’ ili kuweza kusaidia kuwafahamu wateja, na kuwaasa wajasiriamali wanapokopa wakumbuke kulipa kwani uaminifu ni kitu muhimu katika biashara.
“Suala lingine la kulipa kipaumbele ni lile la kuongeza thamani ya mazao wanayoyazalisha na tuache kuwazalishia watu wengine bidhaa wakaenda  kuongezea thamani kidogo tu kama vile kwa kufunga na kuweka nembo ya kibiashara na kuuza kwa bei kubwa,” alisema Dk. Kigoda. 
Aliahidi kuwa Wizara yake iko makini kufanya linalowezekana kushirikiana na wajasiliamali hao kutatua  tatizo hilo la kuuza malighafi badala ya bidhaa iliyoongezwa thamani  ili kuongeza ajira na kupunguza umasikini.

No comments:

Post a Comment