Friday, June 7, 2013

*JE TAIFA STARS KUWAONYESHA TENA UBABE MOROCCO KWAO LEO?


Kikosi cha timu ya Taifa Taifa Stars
************************************************************
Na Boniface Wambura, Marrakech
Taifa Stars inatupa karata yake ya pili ugenini kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia kwa kesho (Juni 8 mwaka huu) kuikabili Morocco (Lions of the Atlas) kwenye Uwanja wa Grand Stade hapa Marrakech, Morocco.

Ilipoteza ya kwanza ugenini dhidi ya Ivory Coast mwaka jana, na kushinda mbili mfululizo nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco. Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Morocco ni ya pili kwa Stars katika uwanja huo ambapo mwaka juzi ilifungwa mabao 3-1.

Washabiki wa Morocco wanaonekana kuikatia tama timu yao yenye pointi mbili tu nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kundi hilo la C ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Tanzania yenye sita. Huo ni mtazamo wa washabiki, lakini kwa upande wa timu inaonekana imepania kujichomoa katika nafasi za chini.

Kwa upande wa Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema timu yake imepania mechi hiyo, lengo likiwa ni kuona inapata matokeo mazuri baada ya dakika 90 za mechi hiyo itakayokuwa chini ya refa Daniel Frazier Bennett wa Afrika Kusini.

Amesema timu yake itacheza kwa umakini na uangalifu kwa vile wanajua wapinzani wao wakicheza mbele ya washabiki wao watakuwa katika shinikizo za kushinda, jambo ambalo wamejiandaa kukabiliana nalo.

Kwa upande wa maandalizi, Kim amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadhamini wa timu hiyo Kilimanjaro Premium Lager wameiandaa vizuri kwani iko kambini kwa wiki tatu sasa na kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan iliyochezwa wiki iliyopita nchini Ethiopia.

Stars iliifunga Morocco mabao 3-1 zilipokutana Machi 24 mwaka huu jijini Dar es Salaa. Lakini zilipokutana hapa Marrakech mara ya mwisho mwaka 2011, Morocco iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kim amesisitiza kuwa kikosi chake kimepania kufanya vizuri katika michuano hii ya mchujo ya Kombe la Dunia, ha hiyo inathibitishwa na matokeo ya timu kadri inavyoendelea kucheza mechi za mashindano.

“Moja ya mipango yetu katika mechi hizi za Kombe la Dunia ni kushinda nyumbani, hilo hadi sasa tumelifanya kwa asilimia 100. Lakini ili tukae vizuri zaidi tumekuja hapa Morocco kwa lengo la kupata matokeo mazuri, ingawa tunajua mechi itakuwa ngumi,” amesema kocha huyo raia wa Denmark.

Kwa hapa Marrakech mechi hiyo imekuwa haizungumzwi mara kwa mara, na kubwa ni kuwa Wamorocco wengi wanaamini kuwa timu yao ambayo hadi sasa ina pointi mbili haina nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano hiyo

No comments:

Post a Comment