Sunday, June 15, 2014

BALOZI SEIF IDDI AWAONYA VIJANA,UKOSEFU WA HESHIMA NDO CHANZO CHA KUJIHUSISHA NA VITENDO VIOVU.

 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi akitoa nasaha katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi za Seti ya Tv NA King’amuzi chake kwa maskani ya CCM ya Nia Njema ya Kijiji cha Fujoni Nyumba ya Ndege.
 Baadhi ya wanachama wa CCM Maskani ya Nia njema Fujoni wakifuatilia hafla ya kukabidhiwa zawadi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Seti ya TV na King’amuzi chake kwa Wanachama  wa Maskani ya CCM ya Nia Njema ya Fujoni Nyumba ya Ndege.
Balozi Seif akikabidhi mchango wa shilingi laki 500,000/- kwa Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika cha maskani ya Nia Nia njema. Bi Ashura Idrissa.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR ZNZ.

                                          Press Release:-
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba ukosefu wa heshima miongoni mwa Vijana ndio sababu kubwa inayotoa mwanya kwa baadhi yao  kujihusisha na vitendo viovu vya  uvunjifu wa amani hapa Nchini.
Alisema ushawishi wanaoupata vijana hao kutoka kwa watu wakorofi wakiwemo baadhi ya Viongozi wa Kidini  huchangia kuleta wasi wasi na kutishia maisha ya kila siku ya Wananchi na Raia wema.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa onyo hilo wakati akizungumza na Wanachama wa CCM wa Maskani ya Nia Njema iliyopo mtaa wa Nyumba ya Ndege Fujoni ndani ya Jimbo la Kitope katika hafla fupi ya kukabidhi  Seti ya TV na King’amuzi chake kwa ajili ya kupata Habari na Burdani.
Alieleza kwamba wapo watu wanaotaka kuiharibu amani ya nchi kwa kuhujumu kwa makusudi wenzao  walioamua kuhubiri amani wakiwaasa wananchi na hasa waumini kuendelea kuwaheshimu Viongozi wao walipo madarakani.
Balozi Seif alisema jamii imekuwa ikishuhudia baadhi ya Viongozi wa Kidini katika madarasa na mihadhara yao wakiendelea kugeuza maneno ya mwenyezi Muungu na badala yake wakihubiri shari na balaa inayoibua cheche ya shari na kuwapa fursa vijana kufanya matendo yaliyo kinyume na maamrisho ya Kidini.
“ Tumekuwa tukishuhudia matendo ya dhara yanayowapata Viongozi wetu wa kidini walioamua kubeba dhima ya kuhubiri amani. Matokeo yake hupatwa na madhila ya kuhujumiwa na hatiame kupata madhara. Mfano wa matendo hayo ni hili la juzi Darajani lililosababisha kupotea kwa roho ya mwenzetu maskini asiyekuwa na hatia yoyote“. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la uimarishwaji  wa vikundi vya ushirika vya saccos Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwahakikishia Wananchi hao kwamba atakuwa  tayari wakati wowote kusimamia  vyema upatikanaji wa mikopo kwa miradi itakayoanzishwa kupitia vikundi vyao.
Alisema Serikali kuu tayari imeshaanzisha mfuko maalum wa uwezeshaji Wananchi Kiuchumi utaotoa fursa ya ukopeshwaji  fedha wana vikundi vya ushirikia ili waweze kutekeleza vyema miradi watakayoanzisha.
“ Hii Mikopo itakayotolewa na Serikali masharti yake makubwa ni kuhakikisha wana vikundi mnarejesha fedha mnazokopeshwa ili katika mzunguuko wa fedha hizo ziweze kusaidia na vikundi vyengine Nchini “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wana CCM hao wa Maskani ya Nia Njema Mwenyekiti wa Wadi ya Fujoni Nd. Mohd Mwindadi alisema wana CCM hao bado wako imara wakiamini kwamba CCM ndio mhimili na msimamizi madhubuti wa amani na utulivu iliyopo Nchi.
Nd. Mohd Mwindad alimuhakikishia Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kwamba wanachama hao wataendelea kuunga mkono msimamo wa Chama chao wa Serikali Mbili  ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hafla hiyo fupi  ilikwenda sambamba na Balozi Seif kukipatia mchango wa Shilingi Laki 500,000/- Kikundi cha Saccos cha Nia Njema cha Maskani hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuendesha  mradi wa Dagaa ili wajikimu Kimapato.
Wakati huo huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif alipata fursa ya kukagua ujenzi wa Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Tawi la Kazole na kuridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Tawi hilo ambao uwezekaji wake umefikia gharama ya shilingi Milioni tatu na laki saba na nusu alizotoa yeye binafsi.
Akizungumza na wana CCM wa Tawi hilo Balozi Seif alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuona jengo hilo linamalizika na kutoa fursa kwa wanachama hao kufanya shughuli zao za chama kwa ufanisi  badala ya kuendelea kukaa chini ya miti.
“ Lengo letu ni kuhakikisha vikao vyetu vyote ikiwemo maandalizi ya mikutano  yetu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa 2015 tunaifanyia ndani ya Ofisi zetu mpya “. Alifahamisha Balozi Seif.
Balozi Seif alikumbusha ahadi yake aliyoitoa kwamba ifikapo mwaka ujao wa 2015 Matawi yote 20 yaliyomo ndani ya Jimbo hilo yatakuwa tayari yameshakamilika ujenzi wake wa Kisasa unaokwenda na agizo la juu la CCM  Makao Makuu la osifi zake kuwa na hadhi inayofanana na chama chenyewe.
Alieleza kwamba ujenzi wa Tawi la CCM la Boma lililobakia hivi sasa unatarajiwa kukamilika rasmi mwishoni mwa mwaka huu wa 2014.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar



No comments:

Post a Comment