Wednesday, June 11, 2014

DCI MNGULU KUONGOZA TIMU YA WAPELELEZI KUCHUNGUZA TUHUMA ZA WIZI KATIKA VYAMA VYA USHIRIKA MKOANI TABORA

MKUU wa Jeshi la Polisi hapa nchini IGP Ernest Mangu ameteua timu ya askari polisi wataochunguza tuhuma za wizi wa fedha za wakulima wa zao la tumbaku katika vyama vya ushirika vya wakulima hao mkoani Tabora. 

 IGP Mangu amemteua Kamishna wa Polisi Issaya Mngulu (pichani) ambaye ni Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai hapa nchini kuongoza timu. 
 Timu hiyo ya upelelezi kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es salaam tayari imewasili mkoani hapa kuanza kazi ya kuchunguza ubadhirifu huo unaofanyika katika vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku. 
 Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mara baada ya kuwasili mkoani hapa Kamishna Mngulu alisema timu imeundwa kutokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la tarehe 7/6/2014 alipokuwa ziarani mkoani hapa baada ya kuguswa na kilio cha wizi mkubwa wa fedha za wakulima wa tumbaku. 
 Mngulu alisema timu hiyo ni maalumu na imekuja mahsusi kwa ajili ya kuchunguza wizi wanaofanyiwa wakulima wa tumbaku kupitia vyama vya msingi mkoani hapa Alifafanua kuwa timu hiyo inaanza kazi mara moja kwa kuchunguza chama kimoja hadi kingine ili kubaini wizi na hujuma zote zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika ambazo zimekuwa kero kwa wakulima wa zao hilo katika mkoa wa Tabora. 
 ‘Natoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Tabora kutoa ushirikiano kwa timu hii mara watakapohitahika ili kuwezesha mafanikio ya kazi hii kwa wakati mwafaka, kazi hii ni ngumu lakini tutaifanikisha kwa ushirikiano wa wananchi na wadau wengine, aliongeza.

No comments:

Post a Comment