Tuesday, June 17, 2014

SERENGETI BOYS & AMAJIMBOS KUCHUANA AZAM COMPLEX JULAI 18

Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Afrika Kusini (Amajimbos) itachezwa Ijumaa, Julai 18 mwaka huu katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys ambayo imeingia moja kwa moja katika raundi ya pili ya michuano hiyo inatarajia kuingia kambini wiki ijayo kwenye hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, na itacheza mechi hiyo kuanzia saa 10 kamili jioni.

Amajimbos kama ilivyo Serengeti Boys imeingia moja katika raundi ya pili pamoja na timu za Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Congo Brazzaville, Ethiopia, Gabon, Ghana, Ivory Coast, Mali, Morocco, Nigeria, Rwanda, Senegal, Tunisia na Zambia.

Mechi ya marudiano itachezwa Afrika Kusini kati ya Agosti 1na 3 mwaka huu. Iwapo Serengeti Boys itafuzu itaingia raundi ya tatu itacheza mechi zake kati ya Septemba 12 na 14 mwaka huu wakati marudiano itakuwa kati ya Septemba 26 na 28 mwaka huu.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment