Tuesday, June 11, 2013

*MZEE TIMOTHY APIYO AFARIKI DUNIA AFRIKA YA KUSINI

Katibu Mkuu wa Zamani Ofisi ya Rais Ikulu,Mzee Timothy Apiyo (pichani), amefariki dunia katika hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa.
Marehemu Mzee Apiyo alikuwa Katibu Mkuu wa Ikulu kwa Kipindi kirefu mpaka alipostaafu na kuhamia Kinyerezi jijini Dar es Salaam. Anatajwa kuwa ni mmoja wa viongozi waandamizi waliokuwa hawana masihara kazini, kiasi hata viongozi serikalini walikuwa wakimheshimu sana.
Mipango ya kuusafirisha mwili wa marehemu Mzee Apiyo inaendelea nasi tutawafahamisha kila hatua kwa kadri tutavyopata ripoti hizo.
Timothy Apiyo, alizaliwa katika wilaya ya Rorya, Tarafa ya Suba, mkoa wa Mara. Alipata elimu ya msingi na sekondari akiwa hapo na mwaka 1959 alijiunga na Chuo Kikuu cha East Afrika na kuchukua digrii ya kilimo.
Baada ya kuhitimu aliingia serikalini wakati huo Tanzania ikiitwa Tanganyika, na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda. Mwaka 1959 alihitumu Makerere na kupangiwa kufanya kazi katika Chuo cha Kilimo cha Ukiliguru.
Mwaka 1960 alihamishiwa wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga kuwa Bwana Shamba wa Wilaya na mwishoni mwa mwaka huo akahamishwa tena kwenda Wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro ambako alikuwa Ofisa Mwandamizi katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga.
Alikaa Ilonga hadi Agosti 1962 ambapo alipata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani katika Chuo Kikuu cha West Virginia ambako alichukuwa digrii ya pili ya Sayansi ya Kilimo na kutunukiwa cheti mwaka 1963.
Baada ya kurejea nchini, mwaka 1964 alipangiwa kufanya kazi Wizara ya Kilimo na baadaye akapelekwa Shinyanga kuwa Ofisa Kilimo wa Mkoa. Desemba 1965 alihamishiwa mkoa wa West Lake (Sasa Bukoba). Na mwakan 1967 akarudishwa wizarani nikiwa Afisa Mipango Mwandamizi.
Mwaka 1968 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mipango Kilimo katika Wizara ya Kilimo na mwaka uliofuata 1969, akawa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Nyumba, Ardhi na Maendeleo Mijini. Novemba 1969 alirudishwa tena Wizara ya Kilimo kuwa Katibu Mkuu na Aprili 1972 akapata uhamisho kwenda kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda.
Aprili 1974 Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Julai 1986 alistaafu kazi

No comments:

Post a Comment